Skip to content

Wito Watolewa kwa Watumishi Kushiriki Mkutano wa Maboresho ya Huduma Serikalini

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

WATAALAMU wa utawala wa umma na usimamizi wa rasilimaliwatu nchini wanatarajiwa kukutana jijini Arusha kujadili mbinu na mikakati ya kuimarisha utoaji wa huduma serikalini, kupitia mkutano mkuu wa pili wa mwaka wa Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala katika Utumishi wa Umma (AAPAM Tanzania Chapter).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa AAPAM Tanzania Chapter, Leila Mavika, amesema mkutano huo utafanyika kuanzia Mei 5 hadi 8, 2026 katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), na utawakutanisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.

Mavika alieleza kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kujadili namna bora ya kuboresha utawala wa umma na usimamizi wa rasilimaliwatu, sambamba na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoathiri ufanisi wa utendaji kazi serikalini.

“Mkutano huu utatoa jukwaa kwa wataalamu kubadilishana uzoefu na kujadili njia bora za kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Mavika.

Aliongeza kuwa mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kufikiri upya utoaji wa huduma kwa umma: Jinsi Serikali inavyoweza kutumia teknolojia kuanzisha huduma bora na zinazolenga wananchi, kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana na changamoto za mazingira.”

Kwa mujibu wa Mavika, maandalizi ya mkutano huo yanafanywa kwa ushirikiano kati ya AAPAM Tanzania Chapter, Jumuiya ya Wataalamu wa Utawala wa Umma na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Tanzania (TAPAHR), pamoja na Mtandao wa Mameneja wa Utawala na Rasilimaliwatu (TPS-HRMnet).

Alifafanua kuwa AAPAM ni taasisi ya kikanda iliyoanzishwa mwaka 1971 kufuatia mkutano wa mawaziri wa utumishi wa umma uliofanyika Freetown, Sierra Leone, ikiwa na dhamira ya kuimarisha utendaji katika sekta ya umma barani Afrika.

“AAPAM Tanzania Chapter inalenga kuwajengea uwezo watumishi wa umma, kufanya tafiti za kitaaluma na kutoa majawabu ya changamoto za kiutawala na usimamizi wa rasilimaliwatu,” alisisitiza.

Katika mkutano huo, mada mbalimbali zitawasilishwa na wataalamu wabobezi, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete.

Aidha, Mavika aliwataka waajiri katika taasisi za umma kuhakikisha wanawawezesha watumishi wao kushiriki mkutano huo ili kunufaika na maarifa mapya yatakayochochea ufanisi wa kazi.

“Ni muhimu kwa waajiri kuwaunga mkono wataalamu wao kushiriki mkutano huu, kwani utachangia kuongeza ujuzi na kuboresha utendaji katika maeneo yao ya kazi,” alisisitiza.

Alibainisha kuwa siku ya mwisho ya mkutano huo, washiriki watapata fursa ya kushiriki shughuli za kuimarisha mshikamano (team building) zitakazofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Kwa ujumla, mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma kwa wananchi nchini na barani Afrika kwa ujumla.