Skip to content

Wadau Ushirika Wakutana Dodoma Kujadili Maboresho ya Sekta

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

SERIKALI imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika sekta ya vyama vya ushirika kwa kuandaa mkutano maalum wa wadau, utakaolenga kujadili hali ya sekta hiyo pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dkt.Benson Ndiege alisema mkutano huo unakusudia kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa ushirika, kulinda maslahi ya wanachama, na kuongeza imani ya wananchi kwa vyama vya ushirika.

Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa chombo madhubuti cha kuchochea maendeleo ya wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Katika mkutano huu, serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania itazindua kampeni maalum ya kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika vyama vya ushirika yenye kaulimbiu isemayo ‘Linda Ushirika, Chagua Uadilifu’,” alisema.

Aliongeza kuwa kampeni hiyo inalenga kujenga msingi imara wa uwajibikaji, haki na utawala bora ndani ya sekta ya ushirika, ili kuhakikisha rasilimali za wanachama zinalindwa na kusimamiwa kwa weledi.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mkutano huo utawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya ushirika, wakiwemo wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika, taasisi za haki, wadau wa ukaguzi, viongozi wa serikali pamoja na watoa huduma wanaohudumia vyama vya ushirika.

Hatua hiyo inatazamwa kuwa chachu mpya ya mageuzi katika sekta ya ushirika nchini, hasa katika kuimarisha uwazi, nidhamu ya matumizi ya rasilimali na uaminifu kwa wanachama.