NA HAFSA GOLO
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Dk.Khalid Salum Mohamed amesema uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume upo tayari kupokea wageni kwa ajili ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwaka 2027.
Dk.Khalid aliyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua uwanja huo na miradi ya maendeleo inayowekezwa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya wageni na timu zitakazoshiriki mashindano ya AFCON.
Alisema uwanja huo umekidhi viwango na vigezo vya kuwapokea wageni watakaoingia kwa ajili ya mashindano ya hayo.
Alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa akibainisha kuwa miundombinu na huduma muhimu zimeimarika kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo litasaidia kuimarisha heshima,utamaduni na silka ya Mzanzibari katika ukarimu wa kuwapokea wageni.
“Hali niliyoikuta hapa ni nzuri na inatia moyo na viongozi wa serikali na wizara yetu tunaendelea kujipanga, kuhakikisha wageni wote watakaokuja nchini wanapata huduma bora na za haraka zenye kukidhi viwango vya kimataifa kupitia viwanja vyetu vya ndege”,alisema.
Katika hatua nyengine Dk.Khalid aliwasisitiza viongozi na watendaji wa sekta ya anga umuhimu wa kutumia fursa hiyo ya mashindano ya Afcon kutangaza utalii wa ndani pamoja na utamaduni.
Hata hivyo aliwataka watumishi wa viwanja vya ndege na wadau wote wa sekta ya usafiri kuongeza maandalizi zaidi hususan katika eneo la huduma kwa wateja usalama na utaribu mahiri wa shughuli zote zitakazogusa eneo hilo la wageni.
Sambamba na hilo,Dk.Khalid alihimiza suala la nidhamu na utoaji wa huduma utakaozingatia busara ,hekima na lugha rafiki kwa wageni na abiria wote wataoingia nchini kupitia viwanja vya ndege.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Badria Attai Masoud alipongeza juhudi zilizochukuliwa na kueleza kuweka utaratibu wa kuweka matangazo ambayo yatatoa ujumbe wa kuonesha wazi tamaduni za Mzanzibari pamoja na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii wa ndani.
Alibainisha eneo jingine linalohitaji kutiliwa mkazo kwa watendaji wanaohusika na utoaji wa huduma kupitia Uwanja wa ndege ni lugha njema ambayo itachochea heshima na utu wa Mzanzibar.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Hamid Haji Machano alisema anaamini mashindano ya AFCON itakuwa ni kichocheo cha kuongeza mageuzi ya kiuchumi na uimarikaji wa upatikanaji wa huduma bora zaidi.
