Skip to content

Makaa ya mawe nyenzo muhimu katika kujenga uchumi – Mavunde

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema makaa ya mawe yanaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kusukuma mbele ajenda ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda, akieleza kuwa rasilimali hiyo ina mchango mkubwa si tu katika uzalishaji wa nishati bali pia katika kuongeza thamani ya madini na malighafi za viwandani.

Amefafanua kuwa matumizi bora ya makaa ya mawe yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, madini na viwanda.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kikao na wadau wa makaa ya mawe kilichofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini, Mavunde alisisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kushirikiana na wadau kwa kusikiliza na kutatua changamoto zao ili sekta hiyo iweze kukua kwa kasi na ufanisi.

Alibainisha kuwa kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe pamoja na kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha zaidi uchumi wa ndani kupitia shughuli za kuongeza thamani.

Katika kikao hicho, wadau waliwasilisha changamoto mbalimbali zikiwemo gharama kubwa za uzalishaji, usafirishaji pamoja na upatikanaji wa masoko,Waziri mavunde aliahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi changamoto hizo kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Aidha, alieleza kuwa mchakato wa kuweka bei elekezi utafanyika kwa ushirikiano wa karibu na wadau wote ili kuhakikisha kunakuwepo na uwiano unaolinda maslahi ya sekta nzima.

Kwa upande wao, wadau wa makaa ya mawe waliipongeza Serikali kwa kuwahusisha katika majadiliano, wakisema hatua hiyo imeongeza uwazi na kuimarisha imani katika uendeshaji wa sekta hiyo,Pia walieleza utayari wao wa kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuchangia zaidi mapato ya Taifa.

Katika kuimarisha uratibu wa sekta, Mavunde aliwahamasisha wadau kuanzisha chama chao kitakachowaunganisha na kurahisisha utatuzi wa changamoto pamoja na kuimarisha ushirikiano miongoni mwao.

Sambamba na hilo, Waziri huyo alitangaza kuwa Kampuni ya A1 Steels Tanzania Ltd imepanga kujenga kiwanda cha chuma jijini Dodoma, ambacho kinatarajiwa kutumia takribani tani 20,000 za makaa ya mawe kwa mwaka,Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mahitaji ya rasilimali hiyo na kufungua fursa zaidi kwa wazalishaji wa ndani.

Mradi huo pia unatarajiwa kuchochea ajira, kuongeza thamani ya madini na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.

Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha azma ya Serikali ya kuifanya sekta ya makaa ya mawe kuwa chachu ya maendeleo ya viwanda nchini, huku ushirikiano kati ya Serikali na wadau ukiendelea kuwa msingi muhimu wa mafanikio yake.