NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi Zanzibar limeeleza kuwa taarifa zinazodaiwa za baadhi ya watu wameshikwa mabega na sehemu zao za siri kutoweka sio za kweli na ni uzushi unaolenga kusababisha taharuki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Kombo Khamis Kombo ilieleza taarifa zilizozagaa hazina ukweli na zinahusisha moja kwa moja na imani za kishirikina hatua ambayo imezua taharuki kubwa katika jamii na kusababisha madhara ikiwa majeruhi na kifo.
Alisema jumla ya matukio 29 yameripotiwa kutokea katika mikoa minne ya Zanzibar, mkoa wa Mjini Magharib matukio 22, Mkoa wa Kusini Unguja tukio moja, Mkoa wa Kusini Pemba matukio matatu na mkoa wa Kaskazini Pemba matukio matatu.
Alisema katika matukio matatu ya Mkoa wa Kaskazini Pemba tukio moja limesababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Hamad Othman Mwalim mwenye umri wa miaka 35 mkazi wa kijiji cha Jojo watuhumiwa watukio hilo tayari wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Aidha alisema jeshi la Polisi linawashikilia jumla ya watuhumiwa 40 na baadhi yao wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo wakabili.
Kamishna huyo alisema kwenye matukio yote hayo yaliripotiwa wahusika waliodai sehemu zao za siri zimepotea, jeshi hilo limewapeleka hospitali na kufanyiwa uchunguzi na madaktari ambao wamethibitisha kuwa sehemu zao za siri zipo na hakuna athari yoyote waliyokua nayo.
Kamishna huyo aliwasihi wananchi kupuuza uvumi huo na kuacha kusambaza taarifa zisizothibitishwa, kwani kufanya hivyo kunaweza kuvuruga amani na utulivu uliopo katika jamii.
Alisisitiza kuwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika katika kusambaza taarifa za uongo kwa makusudi na kutia taharuki katika jamii atachukuliwa hatua za kisheria.
Sambamba na hayo aliiomba jamii kutoa taarifa sahihi pale wanapobaini viashiria vyovyote vya uhalifu, kuacha kuchukua sheria mikononi na kutumia vyanzo rasmi kupata habari zilizo sahihi.
