Skip to content

Sema na Waziri’ Yaimarisha Mawasiliano Kati ya Serikali na Wananchi

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

WIZARI ya Katiba na Sheria imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya Serikali ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kupitia programu maalum ya “SEMA NA WAZIRI”, hatua inayotajwa kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wananchi na uongozi wa wizara hiyo.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Homera alipokuwa akipokea simu za wananchi kupitia Programu hiyo maalumu.

Programu hiyo iliyozinduliwa rasmi Machi 17, 2026, inalenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za kisheria, huku wananchi wakipata fursa ya kuwasilisha malalamiko, maoni na mapendekezo yao moja kwa moja kwa Waziri husika.

Waziri huyo alisema awamu ya pili ya utekelezaji wa programu hiyo ilifanyika Aprili 15, 2026, ambapo wananchi walijitokeza kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazohusu huduma za wizara hiyo.

“Tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma kwa Mteja, tumepokea jumla ya malalamiko 2,277 ambayo tayari yanafanyiwa kazi, na kupitia programu ya SEMA NA WAZIRI tumepokea malalamiko 67,” alisema Waziri huyo.

Alifafanua kuwa malalamiko hayo yanajumuisha migogoro ya ardhi kwa asilimia 31.3, ajira na kazi asilimia 19.4, madai asilimia 13.4, msaada wa kisheria asilimia 7.4, mirathi asilimia 7.4 na mengineyo ikiwemo masuala ya jinai na ukatili wa kijinsia kwa asilimia 21.1.

Kadhalika alisema kuwa kati ya malalamiko 67 yaliyopokelewa kupitia programu hiyo, jumla ya malalamiko 38 sawa na asilimia 56.7 tayari yamepatiwa ufumbuzi, huku malalamiko 29 sawa na asilimia 43.3 yakiendelea kushughulikiwa na wataalamu wa wizara hiyo.

“Ninapenda kuwahakikishia wananchi kuwa Wizara imejipanga kikamilifu kushughulikia malalamiko yote kwa weledi mkubwa, tukiwa na wataalamu wa kutosha wenye uwezo wa kuyafanyia kazi kwa ufanisi,” alisisitiza.

Aidha, alieleza kuwa programu ya SEMA NA WAZIRI ni endelevu na itakuwa ikifanyika mara mbili kwa mwezi, sambamba na utoaji wa mrejesho kwa wananchi kuhusu hatua zilizofikiwa katika utatuzi wa migogoro yao.

Kadhalika aliwataka wananchi kuendelea kutumia jukwaa hilo muhimu kuwasilisha changamoto zao.

“Naomba wananchi wote muendelee kujitokeza kutumia programu hii kuwasilisha maoni, mapendekezo na changamoto zenu, kwani Serikali imejipanga kuhakikisha kila hoja inapatiwa ufumbuzi unaostahili,”alisema.