Skip to content

Zaidi ya Trilioni 774 zatengwa kuimarisha sekta ya sheria nchini

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

SERIKALI imepanga kutumia zaidi ya Shilingi trilioni 774 katika mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuimarisha sekta ya sheria nchini, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

“Naomba wizara yangu iidhinishiwe jumla ya Shilingi 774,789,136,714 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa vipaumbele vilivyopangwa kwa mwaka huo wa fedha,” alisema.

Alieleza kuwa mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimkakati, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025, pamoja na Mpango wa Taifa wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV).

Kwa mujibu wake, lengo kuu ni kujenga sekta ya sheria yenye ufanisi, inayotoa haki kwa wakati na kutumia teknolojia ya kisasa, huku ikiwezesha ukuaji wa uchumi na kuvutia uwekezaji.

Dkt. Homera aliongeza kuwa wizara inalenga kuibadilisha sekta hiyo ili isiwe tu ya kutoa huduma, bali iwe chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa kuhakikisha mifumo ya kisheria inakuwa rafiki kwa uwekezaji.

Katika mwaka huo wa fedha, wizara imepanga kutekeleza maeneo 15 ya kimkakati yatakayolenga kuimarisha utawala bora, upatikanaji wa haki na ufanisi wa taasisi za sheria.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu Katiba, kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi katika ngazi za kata na vijiji, pamoja na kupanua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC).

Hatua hizo zinatarajiwa kuboresha utoaji wa haki, kupunguza migogoro na kuimarisha imani ya wananchi kwa mfumo wa sheria nchini.