Na Saida Issa, Dodoma
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amewahimiza mawakili wa serikali nchini kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utendaji wao ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima inayoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza Jijini Dodoma katika mkutano wa mawakili wa serikali, Dkt. Homera alisema wataalamu hao ni nguzo muhimu katika kutoa ushauri wa kisheria kwa serikali, hasa katika kipindi ambacho taifa linaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Alieleza kuwa serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), hivyo akasisitiza umuhimu wa mawakili kuhakikisha mikataba yote inalinda maslahi ya taifa.
“Ni wajibu wenu kuhakikisha ushauri wa kisheria unakuwa sahihi, hususan katika miradi ya PPP pamoja na sekta za mafuta, gesi na madini, ili kuepusha migogoro inayoweza kuathiri maendeleo ya nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa sekta hizo ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa, hivyo zinahitaji wataalamu wenye uelewa mpana wa sheria za kimataifa na masuala ya uwekezaji.
Waziri huyo pia aliwahimiza mawakili kuendelea kujiendeleza kitaaluma kupitia mafunzo na semina za ndani na nje ya nchi ili kuendana na mabadiliko ya sheria duniani.
Alisema uzoefu wa baadhi ya nchi unaonyesha kuwa matumizi sahihi ya mfumo wa PPP yamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miundombinu kama barabara na reli, akibainisha kuwa Tanzania inaweza kufikia mafanikio hayo iwapo itaimarisha ushauri wa kisheria.
“Sheria ni msingi wa maendeleo endelevu. Bila usimamizi mzuri wa kisheria, miradi mingi inaweza kukumbwa na changamoto au hata kushindwa kutekelezwa,”alisisitiza.
Aidha, aliwataka mawakili hao kutekeleza majukumu yao kwa umakini ili kuepusha hasara kwa serikali inayoweza kusababishwa na uzembe au mapungufu katika usimamizi.

Dkt. Homera aliipongeza TPBA kwa kuendelea kuimarika na kusisitiza umuhimu wa kuijenga taasisi hiyo kwa misingi imara kuanzia ngazi ya chini hadi taifa, ikiwa na mifumo thabiti ya uendeshaji.
Alisema chama hicho kinapaswa kuwa na muundo madhubuti wenye wataalamu na sekretarieti imara ili kiweze kuhudumia wanachama wake na kuchangia maendeleo ya sekta ya sheria nchini.
Pia alipendekeza kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa maendeleo ya TPBA utakaosaidia kukuza ustawi wa wanachama wake kwa muda mrefu.
Dkt. Homera alisisitiza kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuthamini mchango wa mawakili wa serikali katika kulinda utawala wa sheria na kusimamia vyema rasilimali za taifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, alisema mkutano huo unapaswa kuwa chachu ya mageuzi ya sekta ya sheria badala ya kuwa wa kawaida, kwa kuweka msingi wa dira ya maendeleo hadi mwaka 2050.
Alibainisha kuwa mawakili wa serikali wanapaswa kujiona kama sehemu muhimu ya uongozi wa mfumo wa sheria, ambao ni nguzo ya maendeleo ya taifa.
Maswi aliongeza kuwa hata kama taifa lina rasilimali nyingi, haliwezi kupiga hatua bila kuwa na mfumo imara wa sheria unaosimamia matumizi yake.
“Tumekutana hapa si kwa mazoea, bali kujenga msingi mpya wa sekta ya sheria na kuimarisha taasisi zetu ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi kote nchini,” alisema.
Naye Rais wa TPBA, Bavoo Junus, alisema chama hicho kimeendelea kupanuka na sasa kina wanachama zaidi ya 4,600 kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku akieleza kuwa ushirikiano na serikali unaendelea kuimarika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPBA, Addo November, alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana bado kuna changamoto kadhaa za kiutendaji, ikiwemo tofauti za mishahara kwa watumishi kutoka taasisi na halmashauri mbalimbali.
Alisema chama hicho kinaendelea kuwasilisha hoja hiyo serikalini ili kuhakikisha kunakuwa na usawa kazini, huku akiomba pia kuimarishwa kwa mipango ya afya na ustawi wa watumishi ikiwemo programu za mazoezi.
Kwa ujumla, mkutano huo umetajwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili mustakabali wa sekta ya sheria nchini na kuimarisha mchango wa mawakili wa serikali katika maendeleo ya taifa.

