Na Saida Issa, Dodoma
Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, amesisitiza nafasi muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kurahisisha utendaji kazi na kuchochea maendeleo, akibainisha kuwa sekta hiyo imekuwa chachu ya fursa mpya hasa kwa wasichana.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika TEHAMA, Dkt. Mkama amesema dunia imeendelea kuhamasisha ushiriki wa wasichana katika masomo ya teknolojia ili waweze kunufaika na uchumi wa kidigitali unaokua kwa kasi.
Amesema TEHAMA ina mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu, kuongeza ajira na kuchochea ubunifu miongoni mwa vijana, hivyo ni muhimu kwa wasichana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika sekta hiyo.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa shule na vyuo Tanzania Bara na Zanzibar kuanzisha klabu za kidigitali zitakazowawezesha wanafunzi, hususan wasichana, kupata ujuzi wa teknolojia mapema na kujiandaa na ushindani wa kimataifa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mkama amesisitiza haja ya kuwa na mfumo endelevu wa kuwaibua na kuwaendeleza washindi wa mashindano ya TEHAMA ili kuhakikisha vipaji vyao vinatunzwa na kuendelezwa kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Jabiri Bakari, amesema matumizi ya Akili Bandia (AI) yamekuwa yakiongezeka duniani kutokana na maendeleo ya teknolojia na uwezo mkubwa wa mifumo ya kisasa kuchakata taarifa.
Ameeleza kuwa ingawa teknolojia ya AI ilianza tangu miaka ya 1950, kwa sasa imeimarika zaidi na kuwa sehemu muhimu ya huduma nyingi za kidigitali, zikiwemo za mawasiliano ya simu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Ulanga, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea tangu mwaka 2016 za kuongeza uelewa wa TEHAMA nchini, ambapo mwaka huu wanafunzi 281 wamenufaika na mafunzo hayo na 31 kufika ngazi ya kitaifa.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Beatrice Chrispine amewahimiza wasichana kuachana na hofu ya kusoma masomo ya TEHAMA, akisema sekta hiyo ina fursa nyingi za ajira na inaweza hata kumwezesha mtu kujiajiri au kupata kazi kwa urahisi zaidi.

