Skip to content

Vijana kupata nguvu mpya kupitia programu ya Mama Samia

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amezindua rasmi Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi, akihimiza waajiri nchini kuwapa nafasi vijana watakaopitia mpango huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Akizungumza jijini Dodoma baada ya uzinduzi huo, Prof. Mkenda alisema serikali imegharamia kikamilifu utekelezaji wa programu hiyo, hivyo mafundi hawatatakiwa kulipia gharama zozote ili kushiriki.

Alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wake kufanyika kwa kuzingatia misingi ya usawa na uwazi, huku akiitaka VETA kuhakikisha walengwa wote wanafikiwa bila upendeleo.

Prof. Mkenda alieleza kuwa wizara itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na maboresho yake ya mwaka 2023, ambayo yanatilia mkazo maendeleo ya elimu ya ufundi stadi ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Aliongeza kuwa juhudi hizo zinaendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26) unaolenga kukuza rasilimali watu na kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea nguvu kazi yenye ujuzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Wanu Hafidhi Amir, alisema programu hiyo imekuja wakati muafaka, ikilenga kuongeza ushindani wa ujuzi miongoni mwa wananchi na kuwasaidia kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo kushiriki zabuni.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore, alisema jumla ya watu 14,400 wanatarajiwa kufaidika katika hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa mpango huo.

Baadhi ya wanufaika wameeleza kuwa programu hiyo itawasaidia kupata uthibitisho rasmi wa ujuzi wao, jambo litakalowaongezea kujiamini na kuwafungulia milango ya ajira pamoja na fursa kubwa za kiuchumi ambazo hapo awali zilikuwa ngumu kuzipata.