NA KHAMISUU ABDALLAH
MKUU wa Wilaya ya Mjini, Dk. Said Haji Mrisho, amewataka wafanyabiashara wanaojishughulisha na uchongaji wa mbao pamoja na uuzaji wa samani katika eneo la Kijangwani kujiandaa kuhamia katika eneo maalum walilotengewa na Serikali kwa ajili ya shughuli zao.
Akizungumza na wafanyabiashara hao ofisini kwake Amani, Dk. Mrisho alisema hatua hiyo inalenga kuwawekea mazingira bora ya kufanyia kazi bila usumbufu wala hofu.
Alieleza kuwa katika hatua ya mpito, wafanyabiashara hao wataruhusiwa kuendelea na shughuli zao katika eneo la Sebleni, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayewazuia au kuwasumbua.
“Eneo hili tunalowapeleka litabaki kuwa la Serikali, lakini hakuna mtu yeyote atakayekuja kuwabughudhi wala kuwawekea vikwazo,” alisema.
Dk. Mrisho alifafanua kuwa eneo jipya walilotengewa lina miundombinu muhimu ikiwemo vyoo, maji safi na huduma nyingine muhimu, zitakazowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Aliongeza kuwa Serikali haina lengo la kuwaondoa wafanyabiashara hao bila kuwapatia mbadala, bali inalenga kuwainua kiuchumi kwa kuwapatia mazingira rafiki ya biashara.
Aidha, alibainisha kuwa uwepo wa wafanyabiashara hao katika eneo lisilo rasmi umekuwa ukisababisha changamoto mbalimbali, ikiwemo msongamano na ukosefu wa mpangilio mzuri wa shughuli za biashara.
Akizungumzia mpango wa kulipanga upya eneo la Kijangwani, alisema Serikali inalenga kuhakikisha shughuli zote za biashara zinafanyika kwa utaratibu unaozingatia usalama, usafi na maendeleo ya mji kwa ujumla.
“Ni lazima kupanga mji ili wananchi wapate maeneo rasmi ya kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji,” alisisitiza.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Said Kheir Khalfan aliipongeza Serikali kwa kuwajali na kuwapatia eneo hilo maalum kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.
Alisema wafanyabiashara wako tayari kuhamia katika eneo hilo jipya na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuongeza kipato chao pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa.
