WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akil, amesema Zanzibar kwa kiasi kikubwa inategemea ukusanyaji wa mapato ya ndani hususan yatokanayo na kodi, ambayo hutumika kutekeleza miradi ya maendeleo, kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi.
Dk. Akil, ameyasema hayo wakati akizungumza na watendaji wa Benki Kuu ya Tanzania Ofisi ya Zanzibar mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea makao makuu ya Benki hiyo hapa Zanzibar katika ofisi ndogo Kinazini.
Alisema mapato hayo ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa shughuli za serikali na utekelezaji wa mipango ya maendeleo, ambapo alisema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Tume ya Mipango zimebaini kuwa Zanzibar inapoteza zaidi ya asilimia 83 ya mapato ambayo ingeweza kuyakusanya endapo kungekuwa na mifumo imara na ya kisasa ya ukusanyaji.
Alibainisha kuwa upungufu huo unatokana na kutokuwepo kwa mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, hali inayosababisha serikali kukusanya takribani asilimia 17 tu ya uwezo wake halisi.
Dk. Akil alisema endapo mifumo ya kidijitali itatumika kikamilifu, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia asilimia 100 ya makusanyo, hivyo kuziba pengo la upotevu wa mapato unaofikia asilimia 83 ambayo kwa sasa nchi inashindwa kuyakusanya na nchi inapoteza mapato yake.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa uchumi wa kidijitali, alisema ni lazima sekta ya fedha ihakikishe kila senti inakusanywa ipasavyo na kuelekezwa katika malengo yaliyokusudiwa.
Alibainisha kuwa matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali yataiwezesha nchi kujenga miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea kwa kiasi kikubwa mikopo.
“Nchi inaweza kujenga miradi yake mikubwa bila ya kukopa fedha nyingi hivyo BOT endeleeni kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna gani ya kutumia mifumo ya kisasa ya kifedha ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali,” alisema
Dk. Juma alisisitiza kuwa ni lazima nchi iendelee kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo hususan ile ya kimkakati, akibainisha kuwa mapato ya ndani yakikusanywa ipasavyo yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi kwa ujumla.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Benki Kuu katika kuimarisha tafiti na ukusanyaji wa takwimu sahihi ili kuweka mazingira wezeshi ya maendeleo ya kiuchumi kwani kufanya hivyo nchi itaendelea kujenga uchumi imara.
Mapema akitoa taarifa ya utendaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mkurugenzi wa Benki hiyo Ofisi ya Zanzibar, Ibrahim Joseph Malogoi, alisema benki kuu kimsingi jukumu lake ni kutekeleza kazi za msingi za nenki kuu ya Tanzania.
Hata hivyo alisema Benki Kuu inaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi kama mhifadhi na mlipaji mkuu wa SMZ na taasisi nyengine za SMT zinazofanya shughuli zake Zanzibar.
Alisema hadi Disemba 2025 idadi ya benki za biashara zinazofanya kazi Zanzibar ni 15 zenye mtandao wa matawi 43.
Mkurugenzi Ibrahim alibainisha kuwa makao makuu ndogo ya BOT inaendelea kuhifadhi fedha za SMZ zinazotokana na kodi na zisizotokana na kodi na kuipatia serikali hali halisi ya kifedha kila siku ili iweze kufanya maamuzi sahihi ya matumizi.
Majukumu mengine alisema ni kuhaulisha fedha na kutoa vitabu vya hundi kwa wizara na idara mbalimbali za SMZ, kuchambua fedha, kuziweka kwenye mzunguko na nyengine kuziondoa.
Alifahamisha kuwa benki pia hufanya tafiti mbalimbali ikiwemo utafiti wa hali ya uwekezaji Zanzibar, utafiti wa sekta ya utalii, utafiti wa upatikanaji wa chakula na tafiti nyengine.
Alisema katika mwaka huu wa fedha shughuli za miradi mbalimbali ilipangwa kutekelezwa ambapo hadi kufikia Disemba mwaka 2025 benki kuu Zanzibar imeendelea kusambaza fedha (noti na sarafu) ili kutosheleza mahitaji ya uchumi bila kusababisha mabadiliko ya kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma.
Alifahamisha kuwa katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2025 benki kuu ilisambaza jumla ya shilingi bilioni 465.6 kati ya fedha hizo bilioni 394.3 zilisambazwa kupitia ofisi ya Unguja na shilingi bilioni 71.3 kupitia kituo cha Pemba.
Alisema pamoja na mafanikio hayo zipo baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ambazo ni pamoja wananchi kutokuwa na uelewa mzuri kuhusu majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania, kutokuwa na uelewa wa fursa za uwekezaji katika masomo ya kifedha, kutozitambua noti halali na namna bora ya utunzaji wa fedha.
