RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema shughuli zote za nchini zinarejea kama kawaida baada ya maandamano yaliyofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania.
Dk. Samia aliyasema hayo jana mara baada ya kula kiapo cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Chamwino Dodoma.
Alisema kuwa amesikitishwa sana na vurugu zilizotokea jambo ambalo limeipaka matope Tanzania ambao sio utamaduni wake kufanya hivyo.
“Kuanzia leo (jana) shughuli zote zitarudi kama kawaida na kwamba amani, mshikamno na umoja tutaulinda ili kuona kuwa watu wanaishi chini ya utawala wa sheria unaodumisha mshikamano wa taifa”, alisema.
Alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kusimamia usalama wa nchi na kufanya uchunguzi kwa waliosababisha vurugu na kuvunjia kwa baadhi ya maeneo.
Alisema matakwa ya kikatiba ni kuona amani inadumu, mshikamano unaendelezwa na umoja unaimarika jambo ambalo ndilo linalotakiwa kwa Tanzania.
Mapema yeye na viongozi wenziwe waliahidi kulitumikia taifa kwa nguvu zao, maarifa na juhudi zote kuijenga nchi kwa misingi minne ya kuelewana, kustahamiliana, kuvumiliana na kupendana kwa kutochoka wala kurudi nyuma ili kuona maendeleo ya dhati yanafikiwa.
“Uchaguzi umemaliza kazi iliyobaki viongozi waliochaguliwa wote kuhakikisha wanafanya kazi ya kuijenga nchi na kudumisha amani na utulivu na kuleta maendeleo”, alisema.
Aidha, aliwashukuru wananchi na viongozi wote waliompa imani ya kumchagua na kuwataka viongozi wote waliosimamishwa kwenye uchaguzi huo wakiwemo wabunge, wawakilishi na madiwani kuleta maendeleo ya wananchi.
Hata hivyo, alivishukuru vyama vyote 17 vilivyoshiriki kwenye uchaguzi mkuu kwa kuendesha kampeni za kistaarabu, amani na utulivu kwa kipindi chote ambacho walishindana kwa hoja na sera na hatimae wananchi kukipa ridhaa CCM.
Pia aliwashukuru waangalizi wote wa jumuiya za kitaifa na kimataifa wakiwemo kutoka SADC, EAC, nchi za maziwa makuu nakadhalika ambapo walitoa ripoti za awali zilizoeleza kuridhishwa na mchakato wa uchaguzi namna walivyoona.
Rais Samia aliapishwa kushika kipindi cha pili cha urais wa awamu ya sita ambapo atakaa tena madarakani kwa miaka mitano hadi mwaka 2030.
Katika uchaguzi wa Oktoba 29 Rais Samia aliwashinda wagombea wa vyama vyengine 16 vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo kwa kupata asilimia zaidi ya 98 za kura zote zilizopigwa.
