RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema mageuzi ya uchumi na fedha yaliyoanzishwa nchini, yamekuwa msingi muhimu katika kuijenga Zanzibar.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika hafla ya kupongezwa kwa mageuzi ya uchumi na fedha, utoaji wa gawio kwa wawekezaji wa hati fungani ya Zanzibar inayofuata misingi ya kiislam (SUKUK) na uzinduzi wa skimu ya hifadhi ya jamii yenye kufuata misingi ya kislam.
Katika hafla hiyo iliyofanyika ikulu mjini Zanzibar, Dk. Mwinyi alisema mageuzi ya kiuchumi na kifedha yaliyokwenda sambamba na ushirikishwaji wa wananchi kikamilifu yameifanya Zanzibar kupiga hatua za maendeleo.
Alifahamisha kuwa utekelezwaji wa mageuzi hayo uliambatana na uwekaji wa sera za utekelezwaji na mifumo imara ya kisasa ya usimamizi wa fedha za umma.
Dk. Mwinyi alisema Zanzibar inashuhudia matokeo chanya kwenye nyanja mbalimbali ikiwa pamoja na ukuaji wa uchumi ambao umefikiza zaidi ya asilimia 7.2 kwa mwaka.
Alifahamisha kuwa jambo jengine ni ongezeko la uwekezaji wa ndani na nje, kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei kwa wastani wa tarakimu moja, kuongezeka kwa mapato ya ndani kwa asilimia 278 katika kipindi cha miaka mitano.
Alieleza kuwa mageuzi hayo yamejengwa juu ya misingi ya uwajibikaji, uwazi na matumizi ya teknologia za kisasa.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema mwaka 2024, serikali ilizindua Zanzibar SUKUK, ikiwa ni chombo cha kifedha kinachoendeshwa kwa misingi ya sharia ya kiislam ambacho kilipata umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi.
Alisema mwaka 2025 wanashuhudia tukio muhimu la malipo ya kwanza kwa wawekezaji wa Zanzibar SUKUK jambo linalothibitisha ufanisi wa serikali katika kusimamia dhamana zake.
Dk. Mwinyi alisema kupitia SUKUK serikali imepata fedha za kugharamia miradi mbalimbali ya kimkakati, kuimarisha imani kwa wawekezaji na kufungua milango mipya kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa maendeleo ya nchi.
Alisema mafanikio ya uchumi shirikishi hayawezi kipatikana bila ya kuwa na mfumo imara wa bima, hivyo kupitia Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), serikali imeanzisha mfumo wa bima ya kiislam (takaful) ambao utakuwa unatoa huduma za bima kwa msingi wa sharia.
Kwa upande wa afya, Dk. Mwinyi alisema anatambua afya njema kwa wananchi ndio msingi wa ujenzi wa uchumi imara, hivyo serikali imeanzisha mfuko wa bima ya afya Zanzibar ili kuhakikisha kila mzanzibari anapata huduma bila ya kujali kipato chake.
Alisema kupitia mfuko huo huduma za afya zimeanza kupatikana kwa urahisi zaidi, vituo vya afya na hospitali vinapata fedha kwa wakati na wananchi wanapata uhakika wa matibabu bora.
“Yapo mengi yanayosemwa majukwaani sasa mimi nisingependa kuyazungumza kwa sababu sina haja ya kujibu lolote, kwani mtu anapoamua kutunga maneno na kusema bila ya kuwa na ushahidi wa kweli ni mpuuzi hupuuzwa”, alisema.
Sambamba na hayo, alisema serikali imefanya mageuzi makubwa katika mfumo wa hifadhi ya jamii nchini ikiwemo kuimarisha utendaji wa mifuko ya hifadhi na kuhakikisha malipo kwa wastaafu yanafanyika kwa wakati, michango inasimamiwa kwa uwazi na faida zinawanufaisha wanachama.
Kwa kutumia mifumo ya kidijitali watahakikisha wafanyakazi wa umma na binafsi wanasajiliwa na kulindwa dhidi ya changamoto za kiuchumi katika uzee, maradhi na majanga.
Akizungumzia uzinduzi wa skimu ya hifadhi ya jamii yenye kufata misingi ya sharia, alisema hatua hiyo itatoa fursa kwa ZSSF kuwekeza kwenye maeneo yanayofuata misingi ya sharia na hata masuala ya hijja yataweza kufanikiwa kupitia mfuko huo.
Alisema uchumi wowote imara unahitaji taasisi madhubuti za mapato hivyo serikali imefanya mageuzi makubwa katika ukusanyaji wa kodi na kuiimarisha mamlaka ya mapato Zanzibar (ZRA) na mifumo yake yote ya ndani.
Aliipongeza kwa heshima na tuzo alizopewa kwa ishara ya kutambua mchango wa serikali katika kuleta mageuzi ya kifedha na kiuchuni nchini kwani ni matokeo ya ushirikiano wa serikali, sekta binafsi, taasisi za kifedha na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk. Saada Mkuya Salum, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa alivyosimamia mageuzi ya kifedha na kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano.
Alisema ni lazima katika nyanja ya uongozi uwe mbunifu na kufikiri ndani ya muda nae ameyafikia hayo kwani wakati anaingia madarakani utaratibu wa kifedha uliokuwepo sio mzuri.
Akizungumzia uvumi unasemwa na baadhi ya wanasiasa kwamba Zanzibar ilipatiwa fedha dola za kimarekani bilioni kwa ajili ya UVIKO 19, alisema jambo hilo halina ukweli kwani fedha hizo zilitolewa kwa Jamuhuri ya Muungano ambazo ni dola milioni 567.25 na Zanzibar ilipatiwa dola milioni 100 sawa na asilimia 20.
Alibainisha kwamba yapo maneno pia yanasemwa kwamba fedha hizo zimeingia kwenye mifuko ya watu fulani jambo ambalo halina ukweli, hivyo wananchi wanapaswa kupuuza.
Mapema, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Aboud Hassan Mwinyi, alisema katika kipindi cha miaka mitano cha serikali ya awamu ya nane imefanya mageuzi makubwa katika sekta za uchumi na fedha ambayo ndio chimbuko la maendeleo nchini.
