NA LAYLAT KHALFAN, CATHERINE MASOLWA KU
JUMLA ya matukio 642 ya moto yameripotiwa kuanzia Januari hadi Disemba 2025 kwa Unguja na Pemba.
Kati ya matukio hayo 125 yameripotiwa kwa mikoa yote ya Pemba na 517 kwa Unguja ambayo mingi yametokea katika makaazi ya watu.
Akizungumza na gazeti hili, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zima Moto na Uokozi Zanzibar, Haji Pandu Hamad, alisema kuwa karibu matukio hayo yote yamechangiwa na matatizo ya umeme na hivyo kupelekea kuunguza majengo na mali za waathirika.
Hivyo, aliwataka wananchi kuhakikisha kuwa shughuli zote za ufungaji wa mifumo ya umeme katika nyumba zao zinafanywa na mafundi waliothibitishwa na wenye sifa stahiki, sambamba na kufuata viwango vinavyotakiwa ili kuepuka ajali zisizo za lazima.
“Ongezeko la matukio ya moto yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar husababishwa kwa kiasi kikubwa na ufungaji holela wa mifumo ya umeme katika nyumba za makazi bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa”, alisema.
Alisema kuwa baadhi ya wananchi hujihusisha na uwekaji wa ‘fitting’ za umeme kwa kutumia watu wasiokuwa na ujuzi wala vibali maalum kutoka mamlaka husika, jambo linalosababisha hitilafu za umeme na kuongeza hatari ya miripuko ya moto inayohatarisha maisha na mali za wananchi.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za mara kwa mara ikiwemo kufanya ukaguzi wa mifumo ya umeme katika nyumba zao, hususan majengo ya zamani ili kubaini mapema hitilafu zinazoweza kusababisha moto kabla hazijaleta madhara makubwa.
“Mara nyingi kumekuwa na uzembe katika masuala ya umeme unaendelea kuwa chanzo kikuu cha matukio mengi ya moto huku akieleza kuwa matukio hayo yamekuwa yakisababisha hasara kubwa za mali na wakati mwingine kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia”, alisema.
Aliongeza kuwa Jeshi la Zima Moto na Uokozi Zanzibar litaendelea kuimarisha juhudi za kutoa elimu kwa jamii kuhusu usalama wa moto ikiwemo matumizi sahihi ya umeme hata ya gesi, njia za kujikinga na moto pamoja na hatua za awali za kuchukua pindi moto unapotokea.
“Wananchi washirikiane kwa karibu na jeshi hili kwa kutoa taarifa mapema wanapobaini viashiria vya hatari ya moto katika maeneo yao, hatua itakayosaidia kuzuia madhara makubwa kabla hayajatokea,” alisema.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Umeme wa Mamlaka ya Huduma za Udhibiti wa Nishati na Maji (ZURA), Mhandisi Yussuf Mohamed Reja, alisema moja ya sababu kuu za ajali hizo ni matumizi ya waya zisizo na ubora unaotakiwa, hususan waya zenye kiwango kikubwa cha alumini badala ya shaba.
Alisema waya hizo husababisha cheche zinazoweza kuanzisha moto majumbani.
Mhandisi Reja alisema pia baadhi ya mafundi wanaofanya kazi za umeme hawajasajiliwa wala kuthibitishwa kitaalamu, hali inayowafanya kutumia nyaya au vifaa visivyostahili kubeba umeme mkubwa, jambo linaloongeza hatari ya ajali.
“Kutokana na hali hiyo, ZURA imeandaa mpango maalum unaolenga kuwasajili mafundi wa umeme katika madaraja tofauti kulingana na uwezo wao wa kitaalamu”, alisema.
Alisema mafundi hao watapatiwa vibali maalum vya kufanyia kazi, pamoja na kufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha wanazingatia viwango vya usalama.
“Mpango huu utasaidia kupunguza ajali za umeme kwa kiasi kikubwa, kwani kila fundi atalazimika kuthibitishwa kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi,” alisema Mhandisi Reja.
Naye Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Haji Juma Chapa, alisema ajali za umeme zinaendelea kuwasababishia wananchi hasara kubwa ya mali na maisha, huchangiwa na matumizi ya vifaa duni pamoja na kuajiri mafundi wasiokuwa na sifa stahiki.
Aliwatahadharisha wananchi kuepuka kutumia watu wasiokuwa wataalamu katika kufunga mifumo ya umeme majumbani mwao, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kujitafutia majanga yasiyo ya lazima.
Kiujumla tangu kuanza kwa mwaka huu mpya wa 2026, zaidi ya matukio 10 ya moto yametokezea katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
