WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dk. Riziki Pembe Juma, amesema ipo haja ya dhati kwa Wazanzibari kulinda, kuenzi na kuendeleza mila, silka na utamaduni wao ili kuendana na mabadiliko ya dunia bila kupoteza utambulisho wao.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa utamaduni uliofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo, Mjini Zanzibar, Waziri Dk. Pembe alisema Wazanzibari wana utamaduni wao wa kipekee, hivyo wajibu wa kuujenga au kuuvunja upo mikononi mwao wenyewe.
Alisema kuwa utamaduni wa Mzanzibari ni hazina kubwa inayopaswa kulindwa na kuendelezwa, ikiwemo kupitia lugha ya kiswahili, sanaa, pamoja na mila za asili kama upishi wa vyakula vya kitamaduni na mavazi.
Dk. Pembe alisema kila jamii duniani ina tamaduni zake, hivyo ni muhimu Wazanzibari kulinda na kuvitangaza vipengele vyao vya utamaduni kitaifa na kimataifa, huku wakizingatia mabadiliko ya dunia ya sasa.
Aliongeza kuwa sanaa haiwezi kuendelea bila kuwepo kwa misingi imara ya utamaduni hivyo, alisisitiza kuwa wizara imeyasikia yote yaliyowasilishwa kama changamoto na itayafanyia kazi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mattar Zahor Masoud, alisema wizara imejipanga kuendeleza utamaduni wa Zanzibar, hususan lugha ya Kiswahili, na lengo la mkutano huo ni kusikiliza kero za wadau ili kuzifanyia kazi.
“Utamaduni ni sehemu ya historia na hazina ya jamii kukosa mikakati madhubuti ni hatari kwani kunaweza kusababisha kupotea kwa historia na mwelekeo wa maisha,” alisema Mattar.
Aliahidi kuwa wizara itachakata mawazo na mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuyaingiza katika mipango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, pamoja na kuimarisha mawasiliano baina ya wizara na wadau wake.
Naye Kamishna wa Idara ya Utamaduni, Omar Salum, alisema sekta ya utamaduni inajumuisha sekta tatu muhimu ikiwemo Baraza la Sanaa la Zanzibar.
Wadau mbalimbali walitoa maoni yao ambapo Mwakilishi wa Wazee wa Mila, Farid Himid, alisema utamaduni ni uti wa mgongo wa jamii na bila kuuthamini jamii itayumba.
Alisema jitihada za wazee wa awali kudumisha mila na silka zimechangia kuvutia watalii na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Akitolea mfano, Farid alisema kwa sasa kunapotea kwa nguvu baadhi ya mila kama matumizi ya birika la kahawa, mavazi ya kanga kwa watoto, pamoja na vyakula vya asili, na kuomba jitihada za makusudi zichukuliwe kurejesha mila hizo.
Kwa upande wa Baraza la Kiswahili, wajumbe walisema changamoto kubwa ni uhaba wa machapisho ya vitabu vya kiswahili pamoja na urasimu unaozorotesha maendeleo ya lugha hiyo.
Nao Wajasiriamali wa bidhaa za kitamaduni walipendekeza kuanzishwa kwa kituo maalum cha utamaduni Zanzibar kitakachosaidia watoto kujifunza sanaa na mila zao, pamoja na kuwepo kwa sheria zitakazolinda utamaduni na maonyesho ya bidhaa za kitamaduni kama vile kanga na vikoi.
Mwandishi wa vitabu, Ali Mwalimu, alisema waandishi wanapaswa kupewa programu maalum za kuwawezesha kuandika na kuhifadhi masuala ya utamaduni.
Naye Mjumbe wa Baraza la Wazee, Ali Mwinjuma Kirobo, alisema utamaduni wa Mzanzibari ni dhahabu, lakini kwa sasa unatishiwa na athari za utandawazi.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili, Amour Abdallah Khamis, alisema lugha ya kiswahili kwa mtazamo wa kiutamaduni imeanza kupoteza mwelekeo kutokana na changamoto mbalimbali huku akisisitiza kuanza kwa waandishi wa habari katika kuisimamia na kuipa thamani lugha hiyo.
Kwa upande wao, watabibu wa tiba za asili waliiomba wizara kuunda kamati maalum ya tiba asili ili kurasimisha na kuendeleza sekta hiyo huku wakieleza kuwa tiba za asili zina mchango mkubwa katika jamii endapo zitasimamiwa ipasavyo.
