NA MARYAM NASSOR
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Riziki Pembe Juma ameahidi kulivalia njuga suala la upatikanaji wa Sheria Mpya ya Habari Zanzibar.
Dk. Pembe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa sekta ya Habari katika ukumbi wa Zanzibar Social Security Funds (ZSSF) huko Kariakoo Mjini Unguja.
Waziri Pembe, alisema kilio hicho cha wanahabari ni cha muda mrefu na kwamba amekisikia na mchakato wake utafanyika Septemba mwaka huu kwa kuupeleka mswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.
“Tayari nimekabidhiwa nyaraka kadhaa za mswada huo na nimeambiwa ulikuwa umefikishwa katika kikao cha makatibu wakuu na mimi nitahakikisha katika vikao vinavyofuata kuusoma Barazani na milango iko wazi kwa wenye ushauri kwangu”, alisema.
Alisema kuwa, sheria mpya ya Habari ikipatikana itasaidia kuweka mazingira mazuri na misingi imara ya kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha aliwahakikishia wadau wa habari kuwa sheria mpya ya habari itapatikana mapema tu katika uongozi wake, kwani anajua jukumu kubwa la waandishi wa habari ni kufanya kazi zao kwa weledi.
“Tunawashukuru sana kwa maoni yenu, kwani yameonesha dira ya wapi tunataka kuelekea kama wizara na tunaahidi kuyafanyia kazi”, alisema.
Nae, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mattar Zahor Massoud, alisema Wizara hiyo itaweka utaratibu mzuri wa kukutana na wadau na waandishi wa habari kila baada ya mienzi mitatu ili kuwaeleza walipofikia.
Alisema kuwa, mkutano huyo ni maagizo ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi baada ya kuwaapisha viongozi hao na aliwataka kwenda kukutana na wadau na wataalamu wa habari.
“Tumekuwa na utaratibu wa kuwakimbia waandishi wa Habari lakini Wizara yetu sasa itaweka utaratibu mzuri wa Waziri kukutana na waandishi wa Habari”, alisema.
Akijibu, malalamiko ya wamiliki wa vyombo vya habari vya binafsi, alishauri kuunda umoja wao ambao ndiyo utawasimamia na kupeleka malalamiko yao kwa wizara.
Nae, mwandishi wa habari mkongwe hapa Zanzibar, Salim Said Salim alisema kilio chao kikubwa ni kupata sheria mpya na rafiki ya habari kwani iliyopo sasa imepitwa na wakati.
“Tumeanza mchakato wa kudai sheria mpya takriban miaka 20 sasa lengo ni kupata sheria rafiki ya habari bila ya mafanikio yoyote, hivyo tunamatumaini makubwa na waziri Pembe”, alisema Salim.
Kwa upande, wake Mohamed Abdalla mmiliki wa Zanzibar Cable, aliomba kupunguziwa kodi ili kutoa huduma kwa wananchi bila ya mivutano na wahusika wa masuala ya kodi.
Nae, Dk. Imane Duwe alisema wanataka sheria mpya na rafiki ya habari kwa sababu iliyopo sasa ni ya zamani na kwamba haihusishi mitandao ya kijamii na watunga Maudhui ya kimtandao ambayo baadhi inachangamoto zake.
“Tunaomba tupatiwe sheria nzuri na rafiki ya Habari kwa sababu hii iliyopo ni ya zamani na haiendani na wakati wa sasa”, alisema.
Mkutano huo umewakutanisha wadau wa Habari Sanaa, Utamaduni na Michezo, ikiwa ni muendelezo na Maagizo ya Rais Dk. Mwinyi ya kuwataka viongozi aliyowachagua kufanya kazi kwa kuwasikiliza wanaowahudumia.
