RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaapisha viongozi aliowateuwa hivi karibuni.
Hafla ya kuwaapisha viongozi hao ilifanyika jana Ikulu Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, chama na vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Walioapishwa ni Dk. Said Haji Mrisho Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, Lailah Burhan Ngozi, Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, Ali Abdalla Said Natepe Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘B’, Riziki Daniel Yussuf Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja na Zuhura Mgeni Othman Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Wakizungumza mara baada ya kula kiapo viongozi hao walimpongeza Rais wa Zanzibar kwa kuonesha uaminifu wake kwao kuwapa nyadhifa hizo ambazo ni kubwa kwa ajili ya kumsaidia kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kufikia malengo yake.
Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘A’, Lailah Burhan Ngozi, alisema amepewa nafasi hiyo hivyo atahakikisha anakwenda kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni ambazo zimewekwa na kuamini kwamba kwa kushirikiana na watumishi wenzake watakwenda kufanikisha malengo yaliyokusudiwa katika wilaya hiyo.
Lailah alisema kwa vile ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na ilani ya chama ilikuwa inaelekeza nini serikali ifanye hivyo anahisi mtihani aliowatungia wenzake amepewa kuufanyia kazi na kuyatekeleza yote ambayo yameelekezwa katika wilaya husika.
Kwa upande wa migogoro ya ardhi alisema jambo hilo haliepukiki hivyo atahakikisha anakwenda kulifanyia kazi kwa kusikiliza pande zote mbili kwani ndio itakuwa suluhisho.
Naye Dk. Said Haji Mrisho, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, alisema atahakikisha anakisimamia kiapo alichokula na kuhakikisha kwamba yale yote mazuri yaliyofanywa na viongozi waliopita kuyasimamia na yale ambayo hayajafikiwa atayasimamia na kuona yanafanikiwa.
Aliahidi kuwa ataendelea kushirikiana na ngazi zote ili kuhakikisha wilaya hiyo inaendelea kuwa salama na kuangalia vyanzo vyote ikiwemo kuupanga na kusimamia usafi wa mji.
“Tutahakikisha tunakwenda kusimamia Baraza la Manispaa na watendaji kusimamia majukumu yao, pia kuangalia vyanzo vya mapato ambavyo vitakuwa ni nguvu ya kusimamia usafi,” alisema.
Hata hivyo alisema katika kusimamia suala la usafi wataangalia utaratibu wa kutafuta kampuni zenye uwezo zitakazopewa jukumu la kufanya usafi katika mji kwani ndio kitovu kikuu cha utalii wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba, Zuhura Mgeni Othman, aliahidi kuifanyia kazi wilaya hiyo kwa kushirikiana na jamii na watendaji wengine ili kuhakikisha wilaya hiyo inaendelea kuwa mikono salama na kufikia lengo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la maendeleo anayoendelea kuyapeleka katika wilaya hiyo.
Akizungumzia lengo la Rais Mwinyi kuifungua Pemba kiuchumi alisema kutokana na nguvu kubwa zilizoelekezwa katika kisiwa hicho utalii utaimarika kwa kasi kwani tayari Searikali inatanua kiwanja cha ndege na ujenzi wa barabara ambapo utalii utafunguka zaidi.
Ali Abdalla Said Natepe ni Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘B’, alisema anafahamu kuwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya inaongozwa kwa mujibu wa sheria na katiba na hivyo ndivyo vitakavyomuongoza katika utekelezaji wa majukumu yake.
Alisema wilaya ya Magharibi ‘B’ inakua kwa kasi na inakabiliwa na changamoto nyingi, hivyo atahakikisha wanashirikiana pamoja katika kuzipatia ufumbuzi wake kwani kwenye maendeleo lazima changamoto zijitokeze.
Aliahidi kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi katika kutatua changamoto za ardhi zilizopo katika wilaya hiyo na kuona ardhi inatumika vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa.
