Skip to content

Zaidi ya 1.01tr/- zatengwa kuimarisha sekta ya afya Z’bar

  • Zanzibar

NA HAFSA GOLO

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mngereza Mzee Miraji, amesema serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo inatarajia kuwekeza shilingi trilioni 1.016 katika sekta ya afya ili kuimarisha miundombinu na huduma za matibabu kwa wananchi.

Alitoa kauli hiyo katika kikao kazi cha kujadili hali ya nguvu kazi katika sekta ya afya kwa sasa na katika miaka mitano ijayo, kilichofanyika Mombasa.

Mngereza alisema fedha hizo zitatumika kuimarisha miundombinu ya kisasa na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya zinazokidhi viwango vya kimataifa, sambamba na kuendeleza ujenzi wa hospitali za kisasa katika mikoa ya Unguja na Pemba.

Alibainisha kuwa mpango huo unahusisha upanuzi na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, pamoja na ujenzi wa hospitali nne za mikoa Unguja na Pemba.

Aidha, alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Kufundishia na Rufaa ya Binguni itakayogharimu dola milioni 209, pamoja na mpango wa kujenga kituo cha saratani cha kimataifa hapa Zanzibar.

Katika kuhakikisha sekta hiyo inaendana na malengo ya Serikali, alisema Wizara imeamua kufanya utafiti wa nguvu kazi ili kubaini idadi ya wataalamu waliopo na wanaohitajika, sifa zao pamoja na uwezo wao wa kitaaluma.

“Utafiti huu utatusaidia kujua mahitaji halisi ya wataalamu, namna ya kuwazalisha na kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya afya,” alisema.

Alikumbusha kuwa katika miaka mitano iliyopita Serikali imejenga hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa zilizogharimu zaidi ya shilingi bilioni 120 hadi 130.

Mngereza alisisitiza kuwa uwekezaji huo mkubwa wa Serikali unahitaji viongozi na watendaji kuleta matokeo chanya ya kiutendaji na kuhakikisha huduma salama na bora kwa wananchi.

Akizungumzia mageuzi ya utoaji huduma, alisema wananchi wanapaswa kutarajia huduma bora zaidi katika matibabu ya maradhi mbalimbali ikiwemo magonjwa ya moyo na saratani, huku Wizara ikihakikisha uwepo wa madaktari bingwa na wabobezi ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya Zanzibar.

Alisema jitihada hizo zinaungwa mkono na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi, ambaye ameonesha dhamira ya dhati ya kuleta mageuzi katika sekta ya afya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tiba, Dk. Marijani Msafiri, alisema kikao kazi hicho kimeandaliwa kwa mashirikiano kati ya UNICEF na Wizara ya Afya Zanzibar kwa lengo la kufanya tathmini na kuandaa mpango mkakati wa rasilimali watu katika sekta ya afya.

Alisema mpango huo utasaidia kukagua sifa na viwango vya ujuzi wa watendaji wa afya ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa taaluma na vigezo vinavyotakiwa.

Dk. Marijani aliongeza kuwa kutafanyika tathmini maalumu ya viongozi wa vitengo mbalimbali ili kubaini kama wanakidhi vigezo, na pale panapobainika kasoro zitachukuliwa hatua stahiki.

Alieleza kuwa miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha matibabu ya moyo, mifupa na saratani yanapatikana ndani ya nchi, sambamba na kusomesha wataalamu katika vyuo vyenye ubora na vinavyotambulika kimataifa.

“Mpango huu utaonesha wapi kuna mapungufu na kusaidia kurekebisha changamoto zinazochangia kusafirisha wagonjwa kwenda Tanzania bara,” alisema.