Skip to content

ZAHRI kufanya utafiti utekelezaji huduma bima ya afya

  • Zanzibar

WIZARA ya Afya imezindua utafiti wenye lengo la kutathmini utekelezaji wa huduma za bima ya afya, hatua inayolenga kutambua namna serikali inavyotekeleza mpango wa utoaji wa huduma za bima hiyo kwa wananchi.

Akizungumza katika uzinduzi wa utafiti huo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mngereza Mzee Miraji, alisema kufanya hivyo kutaisaidia serikali kuongeza vyanzo vipya hasa kwenye mifumo ya kifedha itakayoiwezesha kugharamia huduma za bima ya afya.

Alisema miaka kadhaa iliyopita mfuko wa bima ya afya ulianza kutoa huduma kwa watumishi wa serikali ambao umeleta mafanikio makubwa jambo lililoisukuma serikali kupitia wizara ya Afya kuongeza wigo wa utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa kawaida.

Alisema miongoni mwa faida za kuanzishwa kwa bima hiyo ni kuona mzunguko wa fedha zinazopatikana katika bima zinarudi serikalini ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuimarisha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.

Dk. Mngereza alisema shilingi milioni 900 zimekusanywa ambazo zimesaidia kuimarisha huduma za afya kwenye vituo vya afya hasa kwa upande wa vifaa tiba kwa tathmini iliyofanywa kwa miezi michache iliyopita kwenye vituo 50 vinavyotumia huduma hiyo licha kukosekana kwa utaratibu mzuri wa upokeaji wa fedha za bima katika baadhi ya vituo.

Alisisitiza kuwa lengo ni kuona utaratibu huo unaendelea katika vituo zaidi ya 152 nchi nzima, hivyo utafiti huo unatarajiwa kutoa muongozo wa kudumu wa kuonesha namna ambavyo serikali itakuwa na uwezo kugharamia sekta ya afya kuanzia sasa na kuendelea.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (ZAHRI), Dk. Mayasa Salum Ali, alisema utafiti huo unatarajiwa kuchukua miezi 18 ambao utaangalia zaidi utekelezaji wa awali wa bima ya Afya Zanzibar kwa kukusanya taarifa kwa wanufaika na watoaji wa huduma hiyo ili kuelewa changamoto zinazowakabili.

Alisema tathmini hiyo itasaidia kuishauri serikali kwa kutoa muelekeo mpya utakaosaidia kuondokana na changamoto zilizopo sasa na kuhakikisha huduma za bima zinaimarika kwa kuwafikia walengwa kwa kupatiwa huduma stahiki na kwa wakati.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkaazi wa pharmaccess Zanzibar, Dk. Faiza Bwanakheri Abasi ambao ndio wadau wakuu wa mradi huo, alisema kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakishirikiana na serikali kupitia wizara ya Afya katika kuimarisha huduma za bima ya afya tokea kuanzishwa kwake.

Alisema tathmini hiyo itasaidia kuongeza nguvu ya kuwafikia wananchi wengi watakaojiunga na mfuko wa bima ya Afya Zanzibar kwa kuhakikisha wanafikiwa na huduma bora wakati wote.

Kikao kazi hicho kimehusisha wizara ya Afya, wizara ya Fedha na Mipango, wamiliki wa hospitali binafsi, wadau wa maendeleo ikiwemo HIPZ na Pharmaccess.