Skip to content

WEMA yajiandaa kwa jambo kubwa siku 100 za Dk. Mwinyi

  • Zanzibar

NA HAFSA GOLO

SERIKALI kupitia wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imesema itakabidhi miradi mikubwa ya maendeleo ya sekta ya elimu kwa wananchi mnamo Febuari 16 mwaka huu.

Zoezi hilo litafanyika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba na kwamba kutafuatia ziara maalumu ya makabidhiano ya miradi hiyo.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khamis Abdalla Said, alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kutimiza siku 100 za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi tangu alipoingia tena madarakani kipindi cha pili.

“Tutakabidhi vifurushi vya Dk. Mwinyi katika ujenzi wa skuli za ghorofa 13 za Unguja na Pemba katika shamra shamra za siku 100 za Rais Dk. Mwinyi”, alieleza katibu.

Aidha, alisema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati madhubuti wa kuimarisha sekta ya elimu kwa kuhakikisha walimu wanapata mazingira bora ya kufanyia kazi pamoja na wanafunzi kupata miundombinu rafiki ya kujifunzia.

Akizungumzia kuhusu miradi hiyo katibu alisema kuwa anaamini kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika sekta ya elimu utaongeza ufanisi wa walimu na kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi jambo litakaloinua kiwango cha elimu na kuandaa kizazi chenye maarifa na ushindani zaidi.

Alibainisha kuwa siku 100 za uongozi wa Dk. Mwinyi katika sekta ya elimu zimeleta mageuzi na ustawi wa elimu hasa upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kujifundishia ikiwemo kuimarika kwa mifumo ya TEHAMA.