MWANAJUMA MMANGA NA SELEMAN TAMBULENGENI
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi, wameeleza kuridhishwa na utatuzi wa changamoto za kero za kijamii, uwajibikaji imara katika ujenzi wa miradi ya maendeleo sambamba na utekelezaji wa ahadi kwa wananchi.
Waliyasema hayo wakati wakijadili hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, wakati akizindua rasmi Baraza la 11 la Wawakilishi Navemba 10 mwaka 2025 katika ukumbi wa baraza hilo Chukwani.
Walisema hatua hiyo imedhihirishia umma kwamba serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wake Dk. Mwinyi iliyodhamiria kuleta mageuzi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii mjini na vijijini.
Mmoja ya wajumbe hao, Bakari Hamad Bakari wa jimbo la Wawi, alisema kuwa hotuba hiyo imegusa moja kwa moja sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, afya, maji, elimu na masuala mengine ya kiuchumi kwa kuwekeza miradi ya ujasiriamali.
Aliipongeza serikali kwa kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji pamoja na kuendeleza sekta ya utalii, wakisema hatua hizo zitachochea ajira na kuongeza mapato ya ndani.
Nae Mwakilishi wa jimbo la Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu, alieleza kuwa hotuba ya Rais imeweka msingi imara wa maendeleo endelevu na kuwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali katika juhudi zake za kuijenga Zanzibar yenye ustawi na maendeleo jumuishi.
