LAYLAT KHALFAN NA MWAJUMA JUMA
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameishauri serikali kuongeza idadi ya wataalamu wa afya katika hospitali na vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za haraka.
Ushauri huo waliutoa katika mkutano wa pili wa baraza la 11 la wawakilishi uliofanyika Chukwani, wakati wakichangia hotuba ya uzinduzi wa baraza iliyotolewa Novemba 10, 2025 na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Wajumbe hao walibainisha kuwa licha ya uwekezaji mkubwa wa serikali katika ujenzi wa miundombinu ya afya, changamoto ya uhaba wa wataalamu bado inakwamisha utoaji wa huduma.
Mwakilishi wa Viti Maalumu, Fatma Ramadhan Mandoba, alisema serikali inafanya juhudi kubwa katika kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya, juhudi ambazo zinapaswa kupongezwa na watu wote.
Alisema katika awamu hii ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi kuna mabadiliko makubwa ya miundombinu hiyo ikiwemo ujenzi wa hospitali na vituo vya afya lakini kuna changamoto ya uhaba wa wataalamu katika hospitali na vituo hivyo.
“Naipongeza serikali kwa kujenga vituo vingi vya afya na hospitali, lakini kuna upungufu wa wataalamu wa afya, naiomba serikali iajiri wataalamu zaidi ili kufanikisha malengo waliyoyakusudia”, alisema Mandoba.
Mandoba aliongeza kuwa wananchi wameitikia kwa wingi kutumia huduma za afya, jambo linalothibitisha kuwa uwekezaji wa serikali unazaa matokeo chanya.
Alisisitiza kuwa kuongeza wataalamu kutasaidia kukidhi mahitaji ya wananchi, kuongeza ufanisi, na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati unaofaa.
Kwa upande wake pia Mwakilishi wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Kusini Pemba, Mariam Said Khamis, alisisitiza umuhimu wa kuongeza wahudumu wa afya ili wananchi wapate huduma za haraka na zenye ubora.
Aidha alisistiza suala la uimarishaji wa vifaa na mafunzo ya wahudumu, zitahakikisha huduma za afya zinakuwa za kudumu, zenye ubora, na zinakidhi mahitaji ya wananchi bila kutegemea hospitali binafsi.
Sambamba na hayo alisifu juhudi za serikali katika kuhakikisha usambazaji wa dawa, vifaa tiba na miundombinu ya kisasa, hatua ambazo zimeongeza morali ya wananchi na kuimarisha uaminifu katika huduma za umma.
Naye mwakilishi wa jimbo la Mkwajuni, Sulubu Kidombo Amour, alipongeza jitihada za Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuimarisha huduma za afya, lakini akabainisha changamoto zinazohusiana na usimamizi wa hospitali.
Alisema kuwa katika hospitali nyingi, wananchi wanakabiliwa na changamoto za tabia zisizofaa za baadhi ya madaktari, ingawa dawa na vifaa vipo.
Hivyo alimshauri waziri wa afya kuhakikisha usimamizi bora ili huduma ziwe na kiwango cha juu.
Aidha, wajumbe waligusia juhudi za wizara ya ujenzi na uchukuzi katika kuendeleza miundombinu ya barabara na hospitali.
Walisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa miradi yote ya afya ili wananchi waendelee kupata huduma za haraka na bora.
Kuhusu sekta Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi walibainisha changamoto katika usimamizi wa miradi ya boti za kibiashara na mpango wa uchumi wa buluu, na kushauri ufuatiliaji wa fedha zilizopatikana ili kuhakikisha malengo ya serikali yanatimizwa.
