NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua dawati maalum la uwezeshaji biashara za Forodha kwa wafanyabiashara wa Kariakoo pekee ili kuharakisha upatikanaji wa huduma za kiforodha kwa wafanyabiashara hao.
Akizindua Dawati hilo jijini Dar es Salaam Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda amesema uzinduzi wa dawati hilo ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati akizindua soko la Kariakoo Februari 08.2026 la kutaka kuwekwa kwa mazingira rahisi ya kufanya biashara.
Alisema lengo la dawati hilo ni kuwezesha na kurahisisha biashara za wafanyabiashara wa Kariakoo ili kuhakikisha biashara zinafanyika kwa urahisi na kwa wakati ikizingatiwa kuwa soko hilo linatoa huduma kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Tanzania.
Mwenda alisema dawati hilo maalum litafanya kazi saa 24 na kuwa wanafanya utaratibu wa Bandari kavu nazo zifanye kazi saa 24 na shughuli zitakazofanyika ni kupokea mizigo, kuikagua na kuitoa mapema baada ya taratibu wa ukaguzi kukamilika.
“Niwahakikishie wafanyabiashara wote kuwa TRA imejipanga kuendelea kutenda haki kwa walipakodi wote na kutoa huduma kwa usawa ili kuleta usawa sokoni” amesema Kamishna Mkuu Mwenda,” alisema.
Kwa upande wake Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, Juma Bakari Hassan alisema dawati hilo litaongeza kasi ya utoaji huduma kwa wafanyabiashara wa Kariakoo ambao asilimia kubwa ya mizigo yao inatumia Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa upande wao baadhi ya Walipakodi waliokwenda kupatiwa huduma akiwemo Nafsa Momba, Hassan Juma na Richard Haule walipongeza kuanzishwa kwa dawati hilo ambalo litawarahisishia kupata huduma za forodha kwa kuwatatulia changamoto ambazo huwa zinajitokeza wakati wa kutoa mizigo.
