Na Saida Issa,Dodoma
UMOJA wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha Tanzania (TAMIU) umeiomba Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya fedha kwa wakopaji, hatua inayolenga kupunguza changamoto zinazokabili sekta hiyo pamoja na kuboresha urejeshaji wa mikopo.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa TAMIU, mwenyekiti wa umoja huo, Juma Mnaka, alisema ukosefu wa elimu sahihi kwa wakopaji ni chanzo kikuu cha matatizo yanayojitokeza katika marejesho ya mikopo.
Alisema wananchi wengi bado wana uelewa mdogo kuhusu dhana ya ukopaji, huku baadhi yao wakichukulia mikopo kama fedha za msaada badala ya mkopo unaopaswa kurejeshwa.
“Changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu, Wengi wanaamini kukopa ni sawa na kupewa fedha bure. Ni wachache wanaotambua kuwa mkopo ni deni linalopaswa kurejeshwa. Wapo wanaokopa kwa sababu tu huduma ipo, wanachukua fedha na kuzitumia bila kuweka mpango wa marejesho,” alisema Mwaka.
Aliongeza kuwa hali hiyo imechangia kuwepo kwa idadi kubwa ya wakopaji huku kiwango cha urejeshaji kikiwa hafifu,Kutokana na hali hiyo, alisisitiza umuhimu wa elimu ya ukopaji kufika hadi ngazi za chini ili wananchi waelewe wajibu wao wanapokopa.
Aidha, Mwaka aliwataka wakopaji kuhakikisha wanakopa kwa malengo maalum na yenye tija ili kuwawezesha kurejesha mikopo yao kwa wakati, akisisitiza kuwa ukopaji si hisani.
Katika hatua nyingine, aliwashauri wananchi kukopa kupitia taasisi zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania ili kuepuka malalamiko ya kuonewa na baadhi ya watoa huduma wasiofuata taratibu, ikiwemo kunyang’anywa mali kinyume cha sheria.
Sambamba na hilo, mwenyekiti huyo alitoa wito kwa watoa huduma ndogo za fedha kujiunga na TAMIU na kujisajili rasmi BOT ili kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo,alisema usajili huo utasaidia kuhakikisha utoaji wa mikopo unafuata miongozo na viwango vilivyowekwa na serikali, ikiwemo viwango vya riba.
Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo akiwemo Abisai Owuocha walitaja changamoto nyingine zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na ongezeko la matapeli na ukosefu wa mifumo inayounganisha taarifa za taasisi za fedha,Walieleza kuwa hali hiyo inachangia wakopaji kukopa katika taasisi zaidi ya moja bila udhibiti, hivyo kusababisha ugumu katika marejesho.
Naye afisa kutoka Idara ya Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa BOT Potamia Mamsery alionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayobainika kutoa huduma hizo bila kufuata sheria na kanuni zilizowekwa.
