NA MWAJUMA MMANGA
WIZARA ya Habari,Sanaa,Utamaduni na Michezo Zanzibar,imesema inaendelea kutoa ruhusa ya viwanja vya michezo kwa utaratibu mzuri lengo kuvitunza viwanja hivyo.
Naibu wa waziri wa wizara hiyo Ali Abdulgullam Hussein,aliyasema hayo huko Chukwani alipokuw akijibu suala la nyongeza lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la Mtambwe Dk. Mohammed Ali Suleiman,aliyetaka kujua juu ya kuwawezesha vijana waliokuwa hawana uwezo wa kulipa viwanja wakati wanapotaka kutumia.
Alisema serikali inatoa ruhusa kwa kila mtu kutumia viwanja,ikiwemo vya Maisara na Mao ambapo hivi karibu katika viwanja vya Mao kulikuwa na ligi ya Mapinduzi Cup kwa upande wa timu za akademi.
Alisema serikali inaendelea kutoa ruhusa kwa viwanja vya Mao ambapo hufanyika mashindano ya mechi za vijana.
Alisema lengo la serikali kutoa ruhusa hiyo ni kuona vijana wanapata nafasi ya kutumia viwanja hivyo na kuonyesha vipaji ili kuwa wachezaji bora wa baadae.
Alisema wana malengo ya kutafuta msimamizi wa viwanja hivyo ili kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kutumia.
Gullam alisema viwanja vya Maisara vilifungwa kwa sababu ujenzi haujakamilika,lakini hivi sasa vimekamilika na vinatumika.
Akijibu suala la msingi,lililouliza na mwakiishi huyo huyo,aliyetaka kujuwa sababu zinazofanya viwanja vya Maisara kufungwa,jambo ambalo linawakosesha vijana kukushindwa kutumika.
Alisema sababu za kutotumika kwa baadhi ya viwanja ni kunatokana na hatua mbalimbali za uwekezaji ,ikiwemo kutokamilika kwa ujenzi,kutokabidhiwa rasmi na kutopangiwa utaratibu wa matumizi na uendeshaji.
Alisema serikali inaendelea kushughulikia hatua hizo na mara baada ya viwanja vinapokamilika hukabidhibiwa na kupangwa utaratibu wa uendeshaji,kufunguliwa pamoja na kutumika kwa madhumuni ya kuwahudumia vijana kama ilivyokusudiwa.
Alikitoa ufafanuzi juu ya viwanja vya Maisara ,alisema viwanja hivyo vitaendelea kutumiwa na wananchi wote wakiwemo waliokuwa wakivitumia kabla ya kufanyiwa marekebisho.
