NA HAFSA GOLO
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharib, Moh’d Abdalla Ali, amesema kuwa sera madhubuti za uwekezaji zimeendelea kuifungua nchi kuwa kimbilio kwa wawekezaji wa ndani na nje hasa katika sekta ya biashara na kifedha.
Akizungumza katika ufunguzi wa maduka manne ya Kampuni ya Airtel huko Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, alisema mazingira rafiki ya uwekezaji yalioandaliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya makampuni mbali mbali ya kimataifa yanayoendesha shughuli zao visiwani.
Alisema kuwa kampuni ya mawasiliano ya Airtel kuwa ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa sera hizo hasa katika miezi ya hivi karibuni jambo ambalo linawapa ari na moyo wa kuwekeza hapa Zanzibar.
“Ndani ya kipindi cha miezi tisa pekee kampuni imefanikiwa kuingiza zaidi ya dola za kimarekani milioni 586 hii ni kutokana na sera madhubuti za uwekezaji hapa Zanzibar”, alisema.
Aliongeza kuwa ndani ya kipindi kama hicho kampuni hiyo imekusanya mapato zaidi ya dola 4,667 ikiwa ni ongezeko la asilimia 24.6.
Akizungumzia kuhusu ongezeko la wateja alisema kwa sasa kampuni ina zaidi ya asilimia 17.3 ya wateja wake duniani kote.
