RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Balozi Amina Mohammed, jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika kando ya mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Samia alielezea dhamira ya Tanzania kutekeleza maguezi ya kiuchumi, utawala na kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa ili kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika sekta za afya, elimu, maji safi na salama, usafi wa mazingira na kupunguza umasikini.
Aidha, alipongeza mchango wa Umoja wa Mataifa na taasisi zake katika jitihada za maendeleo nchini husasani katika nyanja za ushirikiano wa kidiplomasia na msaada wa maendeleo.
Kwa upande wa wake, Balozi Amina,alisema Umoja wa Mataifa unathamini ushirikiano wa karibu uliopo kati ya umoja huo na Tanzania.
Mapema, Rais Samia, alishiriki kikao cha Umoja wa Afrika (AU) kuhusu G20, ambapo viongozi walipokea taarifa ya matokeo ya Mkutano wa Viongozi wa G20 uliofanyika Novemba, 2025.
Kikao hicho kilipokea taarifa iliyowasilishwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambae alifanikiwa kuandaa na kuongoza mkutano wa kwanza wa G20 uliofanyika Afrika na Rais Samia alimpongeza Rais Ramaphosa kwa mafanikio hayo aliyoyaeleza kuwa ni ya kihistoria kwa bara la Afrika.
“Hatua hii ya kihistoria ni fahari kwa Afrika na ni uthibitisho wa kuongezeka kwa ushawishi wa bara letu katika kuunda mijadala ya kimataifa na kutafuta suluhisho za changamoto zinazoikabili dunia”, alisema Dk. Samia.
Akieleza vipaumbele vya Azimio la G20, alisisitiza masuala muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, yakiwemo kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga, kusimamia vyema madeni ya nchi, kuongeza matumizi ya nishati safi, kuongeza thamani ya madini, pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula.
Kuhusu kukabiliana na majanga, alipongeza G20 kwa kuahidi kuongeza juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi, akibainisha kuwa Afrika bado inaathirika Zaidi na majanga ya asili.
Kuhusu uhimilivu wa madeni, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa madeni ili kusaidia nchi za Afrika kuwekeza katika miundombinu, afya na ulinzi wa kijamii pamoja na kupongeza dhamira ya G20 ya kuongeza matumizi ya nishati safi, akisisitiza kuwa ni msingi wa maendeleo, afya bora na ustawi wa jamii.
Akizungumzia sekta ya madini, alisema kupitishwa kwa Mfumo wa G20 wa Madini muhimu kunatoa fursa kwa Afrika kuchakata na kuongeza thamani ya rasilimali zake badala ya kuuza malighafi pekee.
Alibainisha kuwa Tanzania ina madini muhimu kama nikeli (nickel), grafiti na lithiamu, yanayotumika katika teknolojia za kisasa na nishati safi.
Kuhusu usalama wa chakula, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa kilimo na kuwasaidia wakulima wadogo ili kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa chakula.
Alipongeza hatua ya kupatikana kwa uanachama kamili wa Afrika katika G20 pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa ushirikiano wa Afrika katika masuala ya fedha, akisema hatua hizo zinaimarisha nafasi ya bara katika uchumi wa dunia.
Kikao cha AU kilithibitisha kuongezeka kwa sauti ya Afrika katika majukwaa ya kimataifa na dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhisho za changamoto za pamoja za dunia.
Katika hatua nyengine, Rais Dk. Samia ameteuliwa rasmi na Umoja wa Afrika kuwa bingwa wa umoja huo wa masuala ya afya ya mama na mtoto pamoja na afya na haki ya uzazi na jinsia (SRHR).
Uteuzi huo umeidhinishwa katika mkutano wa AU kufuatia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti ya mwaka 2025 ya Kamati ya Wakuu wa nchi na Kituo cha Udhibiti wa Maradhi Afrika (ACDCP) ambapo atahudumu kwenye nafasi hiyo kwa mwaka mmoja.
Kupitia uongozi wake, Dk. Samia ataratibu na kuhamasisha juhudi za nchi wanachama wa AU za kupunguza vifo vya mama na watoto, kuimarisha mifumo ya afya na kulinda haki za afya ya uzazi barani Afrika.
