Na Saida Issa, Dodoma
Mbunge wa Kahama Mjini, Ngailwa Benjamini, ameishauri Serikali kuhakikisha Bajeti ya mwaka 2026/27 inaweka kipaumbele katika sekta muhimu za barabara, kilimo na maji ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, mbunge huyo alisema anatambua kwa kina changamoto zinazoikabili Kahama Mjini, na akaahidi kuzifanyia kazi kwa juhudi na kwa wakati.
Alisisitiza kuwa mojawapo ya changamoto kubwa katika jimbo hilo ni miundombinu ya barabara, huku akiahidi kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Ninazifahamu changamoto katika jimbo langu, na ninaahidi kuzishughulikia kwa wakati. Ninachowaomba wananchi wangu ni wawe na uvumilivu,Serikali yetu inayoongozwa na Dkt. Samia ni sikivu na ina dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi,” alisema Ngailwa.
Aidha, alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kufanya kazi kwa bidii, na kupitia bajeti ijayo, mipango madhubuti imewekwa, hususan katika kuimarisha vyanzo vya mapato ya ndani ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ngailwa alisema kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivyo kwa maendeleo endelevu.
