Na Saida Issa, Dodoma
JAMII imetakiwa kuadhimisha Siku ya Wapendanao kwa kufanya matendo ya huruma kwa watu wasiojiweza, ikiwemo kuwajali wagonjwa mbalimbali hasa wa afya ya akili.
Wito huo unalenga kuifanya siku hiyo kuwa zaidi ya zawadi na sherehe, bali iwe fursa ya kuonyesha upendo wa kweli kwa vitendo vinavyogusa maisha ya wahitaji katika jamii.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma Mjini, SAKINA MBUGI, wakati wa Matembezi ya Valentine ya Huruma yaliyoandaliwa na ETERNAL INTERNATIONAL.
Matembezi hayo yalilenga kuhamasisha utoaji wa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa wa afya ya akili wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbugi alisema upendo wa kweli huanza kwa mtu kujithamini na kuthamini afya za wengine, akisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha makundi yenye uhitaji yanapata faraja na msaada stahiki.
Aliongeza kuwa kuwakumbuka wagonjwa wa afya ya akili ni hatua muhimu ya kupunguza unyanyapaa na kuwajengea matumaini mapya.
Kwa upande wao, waandaaji wa matembezi hayo wamesema lengo ni kuifanya Siku ya Wapendanao kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa jamii, kwa kuhamasisha mshikamano na kujitoa kwa hali na mali kusaidia wahitaji, huku Wakisisitiza kuwa matendo madogo ya huruma yanaweza kuleta tofauti kubwa katika maisha ya wagonjwa na familia zao.
Baadhi ya washiriki wa matembezi hayo wameeleza kuguswa na hali ya wagonjwa wa afya ya akili na kuahidi kuendelea kuwa mabalozi wa upendo na huruma hata baada ya maadhimisho hayo,Wito umetolewa kwa jamii kuendeleza moyo wa kujali na kushirikiana, si tu katika siku maalum, bali kila wakati kwa ustawi wa wote.
