NA MWANDISHI WETU, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema ni jambo muhimu kwa viongozi wa taasisi za serikali zinazojitegemea kupatiwa mafunzo yatakayowajengea uwelewa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ameyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya wakuu wa taasisi zinazojitegemea za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Tume ya Uchaguzi Maisara.
Alisema mafunzo hayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia katika kutekeleza majukumu yao, kutambua muelekeo sahihi wa serikali sambamba na kujengewa uwezo wa kuziongoza taasisi na Idara zao kwa weledi, ufanisi na tija.
Hemed alifahamisha kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo ni hatua nzuri katika kufikia malengo ya serikali yanayoendelea kusisistiza umuhimu wa kujenga rasilimali watu wenye ujuzi, madili, weledi na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya kiutawala, kiuchumi na kiteknolojia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma, Dk. Abduhamid Yahya Mzee, alisema chuo hicho kitaendelea na mpango wake wa kutoa mafunzo kwa watumishi na viongozi wa taasisi mbali mbali ili kuweza kukumbushana, kujadili na kubadilishana uzowefu katika utendaji wa kazi za kila siku.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Balozi, Mhandisi Zena Ahmed Said alisema mafunzo hayo yatakuwa endelevu ambayo yanalenga kuwakumbusha viongozi wa Umma kuwajibika ipasavyo kwa uadilifu na nidhamu katika majukumu yao.
