NA LAYLAT KHALFAN
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) umesema kuwa kila mwanachama ana haki ya kupata fao la kuumia kazini ikiwa atatimiza masharti na vigezo ya fao hilo kwa mujibu wa sheria.
Mfuko huo uliongeza kuwa ni lazima kufuata taratibu za mfuko ili mnufaika kupata stahiki zake kwa wakati.
Rai hiyo ilitolewa na Ofisa wa ZSSF, Masoud Mrisho Sheha, wakati akitoa elimu kwa wafanyakazi wa ofisi za Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar huko Maisara Mjini Unguja.
Masoud alisema kuwa fao hilo ni miongoni mwa mafao mapya ambalo limeanza utekelezaji wake takriban miaka mitatu sasa lakini kumebainika kutokuwa na uelewa kwa baadhi ya wanachama jambo ambalo wengine hukosa satahiki zao ilhali wanalazimika kuzipata.
“Baadhi ya wanachama wanaamini kuwa tunawanyima au tunawachelewesha stahiki zao kwa makusudi, jambo ambalo si sahihi, ukweli ni kwamba kukosekana kwa taarifa sahihi na nyaraka kamili ndiko kunakosababisha ucheleweshaji wa mafao,” alisema Sheha.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa mwanachama kuwasilisha maombi ya fao la kuumia kazini mara tu anaporejea kazini baada ya kukamilisha matibabu, ikiwa ni pamoja na ripoti ya daktari, mwajiri sambamba na kiungo husika cha mwili wa mwanachama alieumia au sehemu ya tukio ambalo hufanyiwa tathmini na ofisa husika wa fao hilo.
Aidha, alifafanua kuwa fao la kuumia kazini hulipwa kwa wafanyakazi waliopata ajali wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kikazi au waliopata maradhi yatokanayo moja kwa moja na mazingira ya kazi.
Aliongeza kuwa matukio yasiyohusiana na majukumu ya kazi hayapo ndani ya wigo wa fidia kwa mujibu wa sheria na kanuni za mfuko.
Sheha aliwataka waajiri kuhakikisha wanazisajili taasisi zao kama wanachama wachangiaji wa mfuko na kuwasajili wafanyakazi wao wote kama wanachama wanufaika huku akieleza kuwa usajili huo ni wa kisheria na unalenga kulinda maslahi ya mfanyakazi na mwajiri kwa pamoja.
Alionya kuwa kutosajili wafanyakazi kunawaweka hatarini kukosa mafao pindi majanga yanapotokea.
Kwa upande wake, Ofisa wa (ZSSF) anayeshughulikia masuala ya misingi ya Sheria ya Kiislamu, Rauhiya Soud Hamed, alisema mfuko umejipanga kuhakikisha unatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa na uwajibikaji kwa mujibu wa sheria.
Alisema lengo kuu la mfuko huo ni kupunguza athari za kijamii na kiuchumi zinazotokana na majanga ya kikazi kwa kutoa fidia stahiki kwa wakati na kwa ufanisi.
Alibainisha kuwa mfumo wa mafao umeundwa kwa kuzingatia uendelevu wa mfuko ili uweze kuhudumia kizazi cha sasa na kijacho bila kuyumbisha uchumi wake.
Rauhiya aliongeza kuwa utoaji wa elimu kwa wanachama ni sehemu ya mkakati wa mfuko wa kuhakikisha kuwa hakuna mwanachama anayekosa haki yake kutokana na kutokujua taratibu.
“ZSSF itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoa mafunzo na semina zitakazowawezesha wafanyakazi na waajiri kuelewa kwa undani mifumo hiyo”, alisema.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa kuendesha mafunzo kutoka Shirika la Magazeti, Rajab Mkasaba, aliipongeza ZSSF kwa juhudi za kuifikia jamii na kutoa elimu ya moja kwa moja kwa wafanyakazi.
Mkasaba alisema mafunzo hayo yaliongeza uelewa kwa kiasi kikubwa kuhusu haki na wajibu wa wanachama, hususan katika suala la madai ya mafao ya kuumia kazini.
Alieleza kuwa maarifa hayo yatawasaidia wafanyakazi kuchukua tahadhari zaidi wanapotekeleza majukumu yao na kufuata taratibu sahihi wanapopatwa na majanga.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa programu za elimu kwa umma, akieleza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi ni msingi wa kuimarisha uhusiano kati ya mfuko na wanachama wake.
Alitoa wito kwa taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kushirikiana na ZSSF ili kuwajengea wafanyakazi uelewa mpana zaidi kuhusu hifadhi ya jamii.
