Skip to content

Dk. Mwinyi: Tutajenga uchumi wa ushindani

NA MWANDISHI, OMPR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali itaendelea kujenga uchumi shindani na jumuishi, hatua ambayo itaifanya Zanzibar kuwa sehemu rafiki kibiashara na kiuwekezaji.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika hafla ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa 17 wa Jumuia Wafanyabiasha Zanzibar (ZNCC).

Alisema katika kukuza biashara na uwekezaji hapa nchini serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imechukua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuimarisha sera ya uwekezaji, kuimarisha miundombinu, kurahisisha taratibu za usajili wa biashara, uwekezaji na kulinda haki maslahi ya wawekezaji.

Alifahamisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa miradi ya uwekezaji 588 yenye thamani za dola za bilioni 6.9 imewekezwa Zanzibar na kuzalisha ajira zipatazo 28,695.

Alisema serikali imedhamiria kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha uendeshaji na ufanisi wa bandari, kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, kuimarisha uhakika wa huduma ya nishati na kuweka mazingira ya biashara na utendaji wa serikali.

Sambamba na hayo, alisema serikali itahakikisha inaimarisha majadiliano ya kudumu katika sekta binafsi ambayo ni njia bora ya kujenga uaminifu, kupunguza migogoro ya kiutendaji na kuimaridha maendeleo ya biashara na uwekezaji.

Dk. Mwinyi alisema serikali inatambua kuwa sekta binafsi ndio injini ya uchumi, hivyo itaendelea kuipa kipaombele ajenda ya kuboresha mazingira ya biashara yatakayowavutia wawekezaji na kuimarisha uzalishaji wa ndani.

Alitoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kuwa mshirika wa serikali kwa kuwekeza katika uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa, kuzingatia ubora wa bidhaa na huduma, kuajiri na kuwajengea uwezo vijana kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati ili kuchangia maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Kazi na Uwekezaji ambaye ni kaimu waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Shariff Ali Shariff alisema serikali itaendelea kuipa nafasi sekta binafsi hasa ikizingatiwa kuwa sekta hiyo ndio muhimuli wa uchumi wa nchi.

Shariff alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na utekelezaji wa sheria ya sekta binafsi ili kuhakikisha inaweka sawa mazingira ya biashara na uwekezaji nchi, sheria ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika kwake.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya Wafanyabiashara Zanzibar, Ali Amour Suleiman, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari na maboresho katika mifumo ya utoaji huduma serikalini hatua zilizoongeza ufanisi na kuimarisha sekta ya Uwekezaji.

Hata hivyo, alisema licha ya mafanikio hayo bado jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kukosekana kwa umeme wa uhakika na kuzorota kwa ufanisi wa bandari za Zanzibar.

Mwenyekiti huyo alisema kukatika kwa umeme kunasababisha hasara katika viwanda, biashara za chakula, sekta ya utalii na huduma za teknolojia, ambapo (ZNCC) imeshauri hatua zichukuliwe kuboresha miundombinu ya umeme.