Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola, na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, wameanza ushirikiano wa pamoja wa kuimarisha na kufufua uzalishaji wa zao la kahawa katika Wilaya ya Moshi, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa zao hilo la kimkakati ambalo kihistoria limekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa wakulima wa eneo hilo, lakini limeendelea kushuka kwa miaka ya hivi karibuni.
Katika kutekeleza dhamira hiyo, viongozi hao wameandaa kikao cha wadau wa sekta ya kahawa kilichowakutanisha taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania, Bodi ya Kahawa Tanzania, vyama vya ushirika, wataalamu wa kilimo na maafisa ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ili kujadili mikakati ya kuongeza uzalishaji wa kahawa ili kufikia malengo ya kitaifa ya kuzalisha zaidi ya tani laki tatu kwa mwaka.

Katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Koola, ameeleza kuwa uzalishaji wa kahawa katika Wilaya ya Moshi bado ni mdogo, akibainisha kuwa hali hiyo inasikitisha kutokana na historia ya Mkoa wa Kilimanjaro kuwa kitovu cha uzalishaji wa zao hilo, huku akisisitiza umuhimu wa wadau kushirikiana kutoa mawazo na mikakati ya kuboresha uzalishaji wa kahawa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Moriss Makoi amewahakikishia wadau kuwa tayari Bilioni 3 zimepatikana kutoka serikalini kwa ajili ya kuboresha mfereji wa Makeresho hivyo utasaidia sana katika shughuli nzima za umwagiliaji.
Katika hatua nyingine wabunge hao wamevitaka vyama vyote 11 vya wakulima yaani AMCOS kuandaa orodha ya madeni wanayodai ili waweze kufatilia ulipaji wa madeni hayo kwa mamlaka husika.

