WAJUMBE wa Urusi na Ukraine ambao walikuwa kwenye duru nyengine ya mazungumzo ya kumaliza vita mjini Geneva chini ya usimamizi wa Marekani, wameeleza kuna matumaini haififu ya kumaliza vita.
Wapatanishi wa Ukraine na Urusi wamehitimisha mjini Geneva, kuwa mazungumzo hayo ya kutafuta amani hayakupiga hatua yoyote ya matumaini ya kumaliza mzozo huo wa vita.
Katika mazungumzo hayo, ikulu ya Kremlin iliwakilishwa na waziri wa zamani wa utamaduni Vladimir Medinsky huku katibu wa usalama wa taifa wa Ukraine Rustem Umerov akiongoza ujumbe wa Kyiv.
Marekani imekuwa ikishinikiza kukomeshwa kwa vita hivyo vilivyodumu kwa takriban miaka minne, lakini hadi sasa imeshindwa kufanikisha makubaliano kati ya Moscow na Kyiv hasa kuhusu suala muhimu la maeneo ambalo ndilo limekuwa kiini cha tatizo.
Duru mbili za awali za mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine huko Abu Dhabi hazikuzaa matunda yoyote, huku chanzo kimoja kilicho karibu na ujumbe wa Urusi kilieleza kwa sharti la kutotajwa jina kuwa mazungumzo ya hivi karibuni yalikuwa magumu mno na yalidumu kwa saa sita.
Katika hotuba yake, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa upande wake alisema yuko tayari kuchukua hatua za haraka kuelekea makubaliano sahihi ya kukomesha vita.
Zelenskiy alikosoa matokeo ya mazungumzo ya siku mbili mjini Geneva kati ya wawakilishi wa Ukraine na Urusi, akisema hayakufikia matarajio, ambapo alitaka mazungumzo ya Geneva yajikite katika kuangazia masuala ya kiutu kama ubadilishanaji wa wafungwa na raia.
Rais huyo alikuwa anataka mazungumzo hayo miongoni mwa mambo mengine yaangazie uwezekano wa kufanyika kwa mkutano kati yake na Rais Vladimir Putin.
Kwa upande wake, rais wa Urusi Vladimir Putin alisema mazungumzo kama hayo ya kukutana ana kwa ana na Zelenskiy yafanyike mjini Moscow tu, jambo ambalo Zelenskiy amelipinga.
Zelenskiy alihoji ikiwa Urusi ina nia thabiti ya kufikia makubaliano ya amani kwani imekuwa ikitoa kipaumbele kwa kufanya mashambulizi ya makombora kuliko kufuata mchakato wa kidiplomasia.
“Hakuna mtu yeyote nchini Ukraine anayeamini kwamba [Putin] atawahi kuwaacha watu wetu, lakini pia hatoyaacha mataifa ya Ulaya, kwa sababu hawezi kuachana na wazo la vita. Anaweza kujiona kama mtu muhimu, lakini kwa kweli, yeye ni mtumwa wa vita.”
Kabla ya mazungumzo hayo kuanza, waziri wa mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiha ameishutumu Urusi kwa kudhoofisha juhudi za amani baada ya kufanya mashambulizi kwa kufyetua makombora 29 na droni 396.
Mamlaka nchini Ukraine zimesema yalisababisha vifo vya watu wasiopungua wanne na kuwajeruhi wengine kadhaa. Kwa upande mwengine Moscow pia imeilaumu Ukraine kwa kufanya shambulio la droni zaidi ya 150.
Siku chache zilizopita, rais wa Marekani alizidisha shinikizo kwa Ukraine kuitaka kufikia makubaliano haraka na Urusi ambayo inadhibiti karibu theluthi moja ya ardhi ya Ukraine ikiwemo rasi ya Crimea, ambayo iliinyakua mnamo mwaka 2014.
Urusi inadhibiti karibu asilimia 20 ya eneo la taifa la Ukraine ikiwa ni pamoja na rasi ya Crimea maeneo ya mkoa wa Donbas mashariki mwa nchi hiyo ambayo yalichukuliwa hata kabla ya uvamizi wa 2022.
Urusi inaitaka Ukraine kuachilia asilimia 20 iliyosalia ya ardhi yake huko Donesk, ambayo Moscow hadi sasa imeshindwa kuikamata, suala ambalo linapingwa na Ukraine.
Uchambuzi mpya wa data kutoka taasisi ya masomo ya vita (ISW), uliofanywa na shirika la habari la Ufaransa (AFP) unaonesha kuwa Ukraine imerejesha eneo la ukubwwa wa kilomita 63 wiki iliyopita.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi, Maria Zakharova alisisitiza alipozungumza na waandishi wa habari kwamba mazungumzo hayo yatazingatia maslahi ya pande zote.
Aliongeza kuwa “siku zote tunapigania hali ya sasa kutatuliwa kwa njia za amani. Tangu 2014, tumetoa wito wa utekelezwaji wa makubaliano ya Minsk hata baada ya 2022, tulisisitiza mara kwa mara kwamba tunaipa kipaumbele suluhu ya kisiasa na kidiplomasia, na hatujawahi kukataa kufanya mazungumzo.”
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine, Andriy Sybiga aliandika kwenye mitandao ya kijamii mapema kwamba Urusi inadhoofisha na kupuuza juhudi za amani baada ya kuwavurumishia mamia ya droni.
Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi ilirusha makombora 29 na droni 396 katika mashambulizi ambayo maafisa wa eneo hilo walisema yalilenga miundombinu muhimu.
Rais Donald Trump wa Marekani anahimiza mataifa hayo kufikia makubaliano ya kuvimaliza vita hivyo vikubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia ingawa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky analalamika kwamba Trump anaishinikiza zaidi nchi yake.
Hata hivyo, Zelensky alisema Trump amekuwa akimshinikiza kuafiki masharti ya makubaliano hayo alisisitiza kuwa nchi yake inatupilia mbali wazo la kuyaachia maeneo ya Donbas ambayo hayajadhibitiwa na Urusi huku akikosoa shinikizo la kujaribu kufikia makubaliano yasiyo na uwiano wala uadilifu.
Urusi ilianzisha uvamizi kamili wa kijeshi kwa jirani yake Ukraine Februari mwaka 2022, na kusababisha maafa na mauaji ya wengi katika kipindi cha miaka minne ya vita.
