NA KHADIJA KHAMIS, WHSUM
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA), hafla inayotarajiwa kufanyika Februari 14 mwaka huu katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip.
Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk. Riziki Pemba Juma, ameeleza hayo mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.
Waziri huyo amesema kufanyika kwa maadhimisho hayo hapa Zanzibar ni faraja kubwa, kwani kutawezesha kukutana na kubadilishana mawazo kwa wataalam na wadau wa lugha hiyo kutoka ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Dk. Caroline Asiimwe, alisema maadhimisho ya miaka 10 kamisheni hiyo yanaashiria hatua muhimu katika historia yake kama muhimili mkuu katika kukuza kiswahili kama lugha ya mawasiliano rasmi ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Dk. Asiimwe alisema miaka 10 tangu kuanzishwa kwa kamisheni hiyo kunatoa fursa muhimu ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana, ushirikiano na wadau na kuweka mikakati wa lugha hiyo kwa Jumuiya ya Afrika na sehemu nyengine duniani.
Akizungumzia kuhusu kaulimbiu, isemayo ‘Muongo wa KAKAMA’, Dk. Asiimwe alisema inalenga kuimarisha utangamano, ubunifu na maendeleo endelevu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
