NA LAYLAT KHALFAN
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar, (ZSSF) unatarajia kuanzisha skim maalum ya sharia itakayotumia misingi ya kiislamu ili kuwawezesha wanachama wake waislamu kwenda hija na umrah kwa anaetaka kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Mfuko huo skimu hiyo iko katika hatua za mwisho ambapo wanachama watalazimika kuchangia takriban mwaka mmoja ili kukidhi vigezo vya kwenda hija kwa kile ambacho kitawezesha kukusanywa na mfuko kwa wanachama wake.
Ofisa wa (ZSSF) anayeshughulikia masuala ya misingi ya Sheria ya Kiislamu, Rauhiya Soud Hamed, alisema mfuko huo unalenga kukuza utamaduni wa kuweka akiba kwa malengo maalumu, ambapo wanachama wataweza kuchangia na baada ya mwaka watalazimika kwenda hija japo kupitia benki nyengine zenye dhamana ya hija au Vikundi vinavyosafirisha hija.
“Mwanachama kama ana kikundi chake au beki yake anakuja anatwambia wao au sisi tunawasiliana nao na kila kitu tunalipia wenyewe na kinachofuata mwanachama ni kwenda hija au umra tu”, alisema.
Akifafanua zaidi Ofisa huyo alisema kuwa mwanachama mwenye kufaidika na skimu hiyo ni yule ambae ametimiza miaka 50 na kwamba atalazmika kukatwa kwa kile alichokichuma na baadae akitaka kustaafu kwa lazima au khiari ni kupigiwa mahesabu kwa alichokitumia kufanya iabada hiyo tukufu kwa waislamu.
Pamoja na mambo mengine lakini, Rauhiya alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwapa fursa wanachama wa ZSSF kuweka akiba maalum itakayowasaidia kugharamia ibada hiyo ya hija na umra.
Hata hivyo, alisema lengo la ZSSF ni kupunguza mzigo wa kifedha wa ghafla sambamba na kuwafanya wanachama kwenda kufanya ibada hiyo wakiwa na nguvu.
“Imebainika kuwa wanachama wetu wanapostaafu wengi wao wanakuwa wagonjwa na hawana nguvu hivyo kuhiji ukiwa na miaka 50 ni wakati sahihi sana na baadae fao lililobaki atalikuta akistaafu kama atakuwa hai”, alisema.
Rauhiya alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya awali, skim hiyo itasimamiwa chini ya sheria na kanuni zitakazotungwa au kufanyiwa marekebisho ili kuruhusu matumizi maalum ya michango ya hiari bila kuathiri uendelevu wa mfuko.
Alisema kuanzishwa kwa skim hiyo kutaleta manufaa kadhaa ikiwemo kuongeza imani ya wanachama kwa mfuko wao wa hifadhi ya jamii.
Alifahamisha kuwa, mpango huo utakuwa ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma za ZSSF zaidi ya mafao ya kawaida kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wanachama wake.
Mfuko huo unawataka wanachama wake kuanza kujasa fomu za kujiunga na skimu hiyo kwa lengo la kuwawezesha kwenda hija kwa anaetaka, sambamba na kutoa elimu kwa wanachama wake ili kupata uelewa wa hilo.
