Skip to content

ZRA yawaita wamiliki vyombo vya moto kusajili nambari mpya

  • Zanzibar

NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imetumia zaidi ya shilingi bilioni 2.6 kugharamia wananchi wake ili kujiunga na mfumo wa kimataifa wa kulinda vyombo vya moto.

Meneja Usajili wa vyombo vya moto na leseni za udereva kutoka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Hanii Mohammed Khamis, aliyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar leo kwenye viwanja vya Mnazi mmoja Mjini Unguja ikiwa ni zoezi la ZRA kusajili vyombo vya moto.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuimarisha mifumo ya usalama barabarani na kuhakikisha Zanzibar inaendana na viwango vya kimataifa vya udhibiti wa vyombo vya moto.

Aidha alisema matumizi hayo yamelenga kuhakikisha wamiliki wa gari, pikipiki na vyombo vyengine vya moto wanapata usajili rasmi unaotambulika kimataifa na kulindwa dhidi ya wizi na uhalifu unaohusiana na vyombo hivyo.

“Mmiliki wa gari wakati wa kubadilisha nambari ri anatakiwa kulipa shilingi 83,420 na vyombo vya maringi mawili ni shilingi 54,850”, alisema.

Alifahamisha kuwa serikali imeamua kuwasaidia wananchi kuingia katika mfumo huu kwa gharama ndogo ili kila mwenye chombo cha moto awe na usalama na utambulisho halali kwani usajili unatakiwa kuwa shilingi 130,000.

“Tayari Tanzania bara wameshaingia kwenye mfumo huu mpya na usajili wa chombo cha moto ni shilingi 500,000, lakini sisi tumepunguza badala ya kuongeza na kama serikali ingekuwa haijalipa basi fedha hizi zilitakiwa kulipwa na wananchi wenyewe,” alisema.

Akizungumzia zoezi hilo alisema kwa sasa mamlaka kupitia mabadiliko ya sheria namba 7 ya usalama barabarani inasimamia zoezi la kubadilisha nambari za magari kutoka kwenye mfumo wa zamani 101 AA na kuingia kwenye mfumo mpya wa nambari zinazoanzia 101 AAA.

Alibainisha kuwa mabadiliko hayo yanatokana na sababu kuu mbili ambayo ni kuongeza ulinzi na usalama wa vyombo vya moto ili kuondosha wimbi kubwa la wizi wa vyombo hivyo.

Alisema mfumo huo mpya wa namba ni wa kimataifa kwani chombo kitakaposajiliwa na kupewa namba yake itaunganishwa moja kwa moja kwenye namba ya gari (chases number) ambayo itakuwa ya kimtandao ‘dijital’.

Hanii aliongeza kuwa iwapo chombo cha mmiliki kitaibiwa na kusafirishwa nchi yoyote, serikali kwa kushirikiana na Polisi wa kimataifa (INTERPOL) wanaweza kukipata chombo hicho kwa kupitia ‘chases number’ na kujulikana kwamba chombo hicho kimesajiliwa Zanzibar na mmiliki wake ni nani.

Aliitaja sababu nyengine kuwa ni pamoja na ZRA ikuanzisha mfumo mpya ambao kila mmiliki wa chombo atakuwa anajiunga na mfumo kwenye simu yake au kwenye komyuta mpakato.

Hata hivyo, alisema mpaka sasa muamko wa zoezi hilo ni mzuri kwani katika vyombo vya magari wameshaingia katika AAB ambapo zaidi ya gari 1,000 tayari zimeshapita huku bajaji na pikipiki zimeshafika 700 AAA ndani ya wiki moja.

Alibainisha kwamba kisheria kulinda chombo cha mtumiaji, namba za zamani hazitakiwi kutumika na hazitambuliki kisheria lakini ZRA itaendelea kutoa huduma hiyo kwa kuwafata wananchi kuwapa elimu na huduma.

Aliwapongeza wananchi kuitikia wito huo na kuwaomba wale walikuwa hawajasajili vyombo vyao kwa nambari mpya kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Mnazi mmoja.

Nao baadhi ya wananchi wameipongeza serikali kwa kuwawekea mfumo huo ambao utasaidia kupunguza uhalifu na kesi nyingi za watu kuibiwa vyombo vya moto.