NA ASYA HASSAN
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Riziki Pembe Juma, amewataka waandishi wa habari kutumia maarifa ya kidijitali na ubunifu katika kazi zao ili kukuza na kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari.
Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, yaliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja, waziri huyo alisema maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya mawasiliano ya dunia yanahitaji waandishi kuwa na maarifa mapya yatakayosaidia kukifanya Kiswahili kiendelee kuwa lugha muhimu ya mawasiliano na maendeleo.
Alisema kuwa Kiswahili si chombo cha mawasiliano pekee, bali ni hazina kubwa inayobeba historia, utamaduni na utambulisho wa jamii ya Watanzania na watu wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Alieleza kuwa kwa takriban miongo sita na zaidi, vyombo mbalimbali vya habari duniani vimekuwa vikitoa matangazo kwa lugha ya Kiswahili, jambo linaloonyesha nguvu na ushawishi wa lugha hiyo katika ulimwengu wa mawasiliano.
Alisema hali hiyo inaweka wajibu mkubwa kwa waandishi wa habari kuhakikisha wanatumia Kiswahili kwa usahihi, ufasaha na ubunifu ili kiendelee kuwa chombo muhimu cha kuelimisha, kuhamasisha na kuunganisha jamii.
Waziri huyo aliongeza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna haja ya kuongeza juhudi za makusudi katika kukuza na kuimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu ndani ya vyombo vya habari.
Alisema dunia ya sasa inaendeshwa na sayansi, teknolojia na ubunifu wa maarifa mapya, hivyo lugha yoyote isiyokwenda sambamba na maendeleo hayo ina uwezekano mkubwa wa kubaki nyuma.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka waandishi wa habari kuhakikisha wanachangia kukifanya Kiswahili kiendelee kukua kwa kuongeza misamiati mipya inayoweza kueleza dhana za kisasa kwa ufasaha.
Alisisitiza kuwa kupitia kalamu zao, vipaza sauti na majukwaa ya kidijitali wanayotumia kila siku, waandishi wana nafasi kubwa ya kukikuza Kiswahili na kukifanya kuwa lugha yenye nguvu katika ulimwengu wa maarifa.
“Kiswahili ni mhimili mkuu wa mawasiliano katika taifa na pia ni nguzo muhimu ya mshikamano wa jamii, lugha hiyo imewaunganisha Watanzania na pia kuwa daraja la mawasiliano kati ya mataifa ya Afrika Mashariki na sehemu nyingine za dunia,” alisema.
Aliongeza kuwa jukumu la kuikuza na kuilinda lugha ya Kiswahili haliishii kwa taasisi moja pekee, bali ni wajibu wa pamoja unaohusisha serikali, wanahabari, wasomi, watafiti na jamii kwa ujumla.
Alisema lugha inapopewa nafasi ya kutumika katika nyanja mbalimbali za maisha kama elimu, utawala, biashara na teknolojia, huendelea kukua na kuimarika zaidi.
Sambamba na hayo Waziri huyo alitumia fursa hiyo kuwataka waandishi kusimama imara katika kuandika na kuripoti habari zenye usahihi, mizani na uelewa mpana ili kujiepusha na upotoshaji wa taarifa kwa jamii.
Alisema jamii inaitegemea sana sekta ya habari katika kupata taarifa sahihi, hivyo wanahabari wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazotoa zinahamasisha maendeleo na kuimarisha uhusiano kati ya serikali na wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, Mwanahija Ali Juma, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Alisema kupitia mafunzo hayo wanahabari watapata fursa ya kuongeza maarifa yao ya uandishi na kujenga misingi imara inayozingatia matumizi sahihi, fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili.
Alifafanua kuwa hatua hiyo pia inalenga kuchochea maendeleo ya lugha ya Kiswahili katika vyombo vya habari na katika jamii kwa ujumla.
Akiwasilisha mada kuhusu uakifishaji wa alama na vituo vya uandishi, katika mafunzo hayo, Mratibu wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, Zakia Mustafa Fatawi, alisema mada hiyo inalenga kuwasaidia wanahabari kuelewa kwa kina matumizi sahihi ya alama za uandishi ili kuongeza ubora na uelewa wa maandishi yao.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Baraza la Kiswahili Zanzibar na yamelengwa kuwafikia baadhi ya wanahabari wa Unguja na Pemba ambapo pamoja na mambo mengine lakini yanalengo la kuwafunza Kiswahili kwenye uandishi.
