KIASI cha wageni 656,865 wameingia nchini kutoka Januari hadi Septemba 2025, hali inayonyesha maratajio ya serikali ya kufikia lengo la idadi ya wageni 800,000 mwaka huu.
Idadi hiyo imechapuzwa na wageni 84,154 waliongia Septemba ikiwa ni ongezeko la asilimia 38.6 kutoka wageni 60,731 waliongia nchini Septemba, 2024.
Hayo yamebainishwa wakati wa uwasilishaji wa takwimu za uingiaji wa wageni kwa Septemba 2025, hafla iliyofanyika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mazizini jana.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Ofisa Tafiti na Takwimu Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hassan Ame Vuai, alisema, idadi ya wageni walioingia Septemba 2025 ni kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano kutoka Septemba 2021.
Aliitaja Italia ndiyo iliyoongoza kwa kuleta wageni 8,889 sawa na asilimia 10.6, ikifuatiwa na Ujerumani iliyokuwa na wageni 8,698 (asilimia 10.3).
Mataifa mengine ni Uingereza iliyoleta wageni 7,987 (9.5%), Ufaransa wageni 5,940 (7.1%) na Poland wageni 4,475 (5.3%).
Alisema, wageni 55,780 waliingia nchini kutoka Bara la Ulaya sawa na asilimia 66.3, Afrika (13,294), Asia (9,026) na Oceania (906).
Alisema, wageni 77,151 sawa na asilimia 91.7 waliingia kupitia viwanja vya ndege na wageni 7,003 sawa na asilimia 8.3 walipitia bandarini.
Wageni 38,077 walikuwa jinsi ya kiume na 46.077 walikuwa jinsi ya kike huku wageni hao wakikaa nchini kwa wastani wa siku nane.
Mkufunzi Mwandamizi Skuli ya Biashara, Dk. Estella Ngoma Hassan, alisema, Zanzibar bado ina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuongeza idadi ya watalii ikiwemo michezo ya kiutalii na makongamano ya kimataifa.
Alisema, bado wadau wa utalii wanawajibika kuendelea kuitangaza sekta hiyo ili kuondokana na utalii wa msimu na badala yake uwe utalii wa muda wote sambamba na kuongeza masoko mashariki ya mbali.
Aidha, alisema, kuongezeka kwa idadi ya wageni kuendane na ubinifu wa vivutio vingi vitakavyowashawishi kutumia muda mwingi wa kuwepo nchini ili kuongeza mapato.
Meneja Tehama Shirika la Bima Zanzibar, Bakar Mussa Yussuf, alisema, ZIC inajivunia uitikiaji mkubwa wa wageni katika kupata huduma hiyo, licha ya kuwepo changamoto chache ambazo tayari zimeshapatiwa ufumbuzi.
Alisema, ZIC imefanikiwa kupatiwa huduma za kimatibabu wageni 21, wakiwemo saba waliopata ajali ya barabarani na kuhudumiwa kwa ufanisi matibabu yao katika Hospitali ya Lumumba.
