Skip to content

Wafanyabiashara Mwanakwerekwe watakiwa kuhamia soko jipya

  • Zanzibar

NA HAFSA GOLO

MKUU wa mkoa wa Mjini Magharibi, Moh’d Ali Abdalla, amewataka wafanyabiashara wa Soko la Mombasa waliokuwa wakifanya shughuli zao katika eneo la Mwanakwerekwe kupisha ujenzi, kurejea mara moja katika soko hilo kufuatia kukamilika kwa ujenzi wake.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo la Mwanakwerekwe na kuzungumzo na wafanyabiashara ambao bado hawajahamia katika soko jipya, Mkuu huyo wa Mkoa alisema serikali imekamilisha ujenzi wa soko hilo hivyo wafanyabiashara wote wanapaswa kuanza rasmi shughuli zao hapo.

Alieleza kuwa baada ya siku mbili kuanzia jana eneo la Mwanakwerekwe halitaruhusiwa kutumika kwa shughuli za biashara hivyo wafanyabiashara watatakiwa kuliacha wazi eneo hilo na watakaokaidi watachukuliwa hatua.

Akiwa katika soko la Mombasa, Moh’d alieleza kuridhishwa na hatua ya baadhi ya wafanyabiashara kuendelea na biashara zao baada ya kuhamia sokoni hilo la kisasa, huku akiwataka kuzingatia usafi na mpangilio mzuri wa bidhaa.

Aidha aliwasisitiza wafanyabiashara hao kuepuka kuweka bidhaa chini, akieleza kuwa hali hiyo haileti taswira nzuri kwa wafanyabiashara wala wateja wanaofika sokoni hapo.

Kuhusu upatikanaji wa futari katika kipindi cha mezi mtukufu wa ramadhani, aliwasisitiza wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa kwa kisingizio cha kodi, akifafanua kuwa viwango vya kodi vilivyowekwa havisababishi ongezeko la bei ya bidhaa.

Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara waliohamia kwenye soko hilo walieleza kufurahishwa na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwawekea mazingira bora ya kufanyia biashara.

Hata hivyo, waliiomba serikali ya mkoa wa Mjini Magharibi kuwapatia ufumbuzi wa changamoto ndogo ndogo zinazowakabili, ikiwemo kuimarishwa kwa ulinzi pamoja na ujenzi wa mapaa katika maeneo ya wazi ili kuzuia uharibifu wa bidhaa zao.