NA VICTORIA GODFREY
SERIKALI imesema uwanja wa Uhuru (shamba la bibi) utakamilika na kukabidhiwa kabla ya Novemba 21 mwaka huu.
Tayari Serikali imemuogeza fedha mkandarasi ili kuhakikisha anafanya haraka na kukamilisha kwa wakati, uweze kutumikia kwa ajili ya maandalizi ya matukio mbalimbali ya kitaifa yajayo.
Akizungumza katika ziara yake ya ukaguzi uwanja huo Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema hadi sasa umefikia asilimia 90 ya ukarabati.
Alisema uwanja huo utakuwa mbadala kwa kutumika michezo ya kimataifa na ligi kuu ambapo uwanja wa Benjamini Mkapa utakuwa katika matengenezo.
“Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu ukarabati huo ili kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa, na lengo ni kuona uwanja huu unarejea katika hadhi yake” alisema Msigwa.
Aliongeza kuwa kati ya maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni pamoja na ufungaji wa taa mpya za kisasa, uwekaji wa nyasi bora za bandia (Pitch), Paa la uwanja marekebisho ya njia za kukimbilia (Running Track), ufungaji wa viti vipya, ukarabati wa vyoo, ufungaji wa milango mipya na uwekaji wa vigae vipya pembezoni mwa uwanja.
Ukarabati wa Uwanja wa Uhuru ni sehemu ya mipango ya serikali wa kuimarisha viwanja vya michezo nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya sita chini ya Dk. Samia Suluhu Hassan ya kufanya michezo kuwa nyezo ya ajira na uchumi.
