Skip to content

Usafi wa Mazingira Huchangia afya bora, ustawi wa jamii, maendeleo ya kiuchumi

  • Makala

NA RAJAB MKASABA

USAFI ni jambo muhimu, linalotazamwa kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, nyumbani, ofisini, jamii ama taifa na watu wanaoishi kwenye eneo safi kwa mujibu wa wataalamu wanatajwa kuwa na maisha marefu zaidi kuliko wale wanaoishi kwenye mazingira machafu.

Mazingira safi ni nguzo muhimu ya afya ya jamii, maendeleo ya kiuchumi na maisha bora ya kila siku ya mwaadamu yanahitaji usafi.

Mazingira safi hupunguza uwezekano wa bakteria, virusi, na vijidudu vingine hatari kusambaa na hivyo kulinda afya ya wanajamii ambapo pia, usafi wa mazingira hupunguza uchafu unaoingia kwenye vyanzo vya maji kama vile mito, maziwa na visima.

Eneo ambalo ni safi na limepangwa vizuri huwa na mvuto zaidi kwa wakazi na biashara kwani kwa kufanya usafi wa mazingira, thamani ya ardhi na mali inapanda na hivyo kuvutia biashara na hata uwekezaji hatua ambayo huongeza ajira na kukuza uchumi wa eneo husika.

Usafi wa mazingira unahusisha mpangilio bora wa kuhifadhi taka kwa kutumia utaratibu wa kuzichambua, kuchakata, na kutumia tena hatua ambayo husaidia kupunguza rasilimali zinazopotea na kupunguza taka zinazokwenda katika majaa hivyo kupunguza uchafuzi wa ardhi na mabadiliko ya tabianchi.

Mazingira safi yanaonekana kuvutia na huchangia katika kuleta hisia nzuri kwa watu ambapo sehemu zenye usafi huimarisha mandhari ya asili na kuleta uzuri wa mazingira ambayo ni kivutio kwa watu na wageni wanaotembelea.

Mazingira safi katika maeneo ya kazi huongeza tija na morali ya wafanyakazi ambapo wafanyakazi wanaofanya kazi katika mazingira safi na salama wanaweza kufanikisha majukumu yao kwa ufanisi zaidi, na kufanya kampuni au taasisi kufikia malengo iliyojiwekea.

Aidha, mazingira safi huvutia watalii ambao huja kufurahia mandhari nzuri na mazingira ya kuvutia kwani kama inavyofahamika kwamba utalii ni chanzo cha mapato kwa nchi nyingi, hivyo usafi wa mazingira ni muhimu ili kuvutia watalii wengi zaidi ambao huongeza kipato cha taifa na kuboresha maisha ya wanajamii.

Kusimamia usafi wa mazingira hufundisha jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kutunza rasilimali za asili ambapo watoto na vijana wanapoona wazazi na viongozi wakijihusisha na shughuli za utunzaji wa mazingira huwa wanapata funzo la kuendeleza desturi hiyo.

Mazingira safi na yenye utulivu yanaweza kusaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuleta hisia za furaha kwani watu wanaoishi katika mazingira safi wanapata utulivu wa akili na wanaweza kufurahia mazingira yao bila wasiwasi wa afya au usalama.

Mazingira safi yanahamasisha watu kufanya kazi kwa bidii na ari ambapo watu wanapokuwa kwenye mazingira yanayoonekana vizuri, wanapata nguvu na motisha ya kufanikisha shughuli zao za kila siku kwa ufanisi zaidi.

Utamaduni wa kutupa taka ovyo katika eneo lolote lile ambalo halijatengwa na taasisi husika umezoeleka katika miji yetu hali ambayo haileti taswira nzuri.

Baadhi ya wananchi wasiojielewa wala kuelewa umuhimu wa afya zao na wenzao wamekuwa wakitupa taka ovyo, wanamwaga maji machafu ovyo, mitaro ya maji machafu wanaielekeza kwenye mito ama misingi inayopitisha maji na wengine hawachimbi karo za nyumba zao.

Sasa hili ni tatizo kubwa na imekuwa usumbufu mkubwa kwa baadhi ya maeneo kwani wakati mwengine taasisi husika hulisimamia jambo hili lakini wananchi wengine wamekuwa wakaidi licha ya kulipizwa faini.

Kuna baadhi ya wananchi ambao huwemo ndani ya vyombo vya moto kama vile gari hivyo hunywa maji au hula vyakula na baadae maganda ama chupa huzitupa barabarani kwa makusudi jambo ambalo sio busara na linachangia uchafuzi wa mazingira.

Pia, imezoeleka kwa baadhi ya watu ambao hufanya haja ndogo katika vichochoro vya nyumba katika maeneo ya miji yetu jambo ambalo halileti taswira nzuri na pia ni uchafuzi wa mazingira sambamba na kukarisha maradhi.

Kuziba kwa makaro na kupelekea kumwaga maji machafu ni jambo la kawaida kwa baadhi ya maeneo hasa yale ya nyumba za maendeleo hali ambayo husababisha uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa na kuondoa haiba ya mji.

Juhudi zimekuwa zikichukuliwa na taasisi husika licha baadhi ya wakati maeneo huchukua muda kufanyia marekebisho lakini jambo muhimu ni kwa jamii yenyewe kuhakikisha inalisimamia jambo la usafi wa mazingira.

Tuwaunge mkono viongozi wetu wanaosisitiza kila siku suala la usafi katika mazingira yetu hasa ikizingatiwa kwamba nchi yetu ni ya visiwa ambavyo ni kivutio kikubwa cha watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Jamii inapaswa kuhamasishwa kushiriki katika shughuli za usafi wa maeneo ya umma kama vile masoko, skuli na hospitali hatua hii itasaidia kuhakikisha kuwa maeneo haya yanabaki safi na yenye afya kwa matumizi ya jamii nzima.

Kuweka mimea, miti, na mabwawa ya asili katika mazingira ya miji na vijijini husaidia kudhibiti uchafuzi wa maji na hewa kwani miti na mimea husaidia kuchuja uchafu kwenye hewa, huku mabwawa ya asili yakisaidia kuchuja maji taka kabla hayajaingia katika mifumo ya maji ya asili.

Usafi wa mazingira ni jambo la msingi ambalo linachangia afya, ustawi wa kijamii na maendeleo ya kiuchumi ya jamii yoyote kwani mazingira safi yanaimarisha afya ya watu, huongeza uzuri wa mazingira, na huleta furaha ya kihisia na kiakili.

Kila mmoja anapaswa kuchukua jukumu la kutunza na kuhifadhi usafi wa mazingira kwa faida za sasa na za kizazi kijacho pia ni jukumu letu sote kuhakikisha mazingira yetu yanabaki safi na salama kwa faida ya wote.

Nchi ambazo zina hewa safi zaidi haziwi kwenye hatari ya kuwa na mazalia ya wadudu ambao wanaweza kusabababisha magonjwa ambayo yana uhusiano na uchafuzi wa hali ya hewa kwa mfano magonjwa mbalimbali ya mfumo wa upumuaji au magonjwa ya moyo.

Aidha, nchi ambazo zina kiwango kikubwa cha uchafuzi wa hali ya hewa ziko hatarini zaidi kuwa na viwango vikubwa vya magonjwa yasiyokuambukizwa na kuchangia asilimia 72% ya vifo vyote, asilimia 16 katika vifo hivyo vinachangiwa na sumu inayotokana na uchafuzi wa hali ya hewa.

Watafiti kutoka Chuo kikuu cha Yale na Columbia wakishirikiana na ‘World Economic Forum’ wamefanya tathimini ya usafi na mazingira kwa nchi zaidi ya 180 duniani ambapo vigezo mbalimbali muhimu vinazingatiwa kupata orodha ya nchi safi duniani kwa mfano hewa safi, maji safi, usafi wa mazingira, bioanuwai, makazi ya watu na sera endelevu za kuhifadhi mazingira.

Rwanda imetajwa kuwa ni nchi yenye kuongoza kwa usafi barani Afrika kwa miaka mine mfulululizo ambapo baada ya kukumbwa na vita na mauaji ya kimbari katika mwaka 1994, imerejea na kuweka nguvu kwenye kujijenga na kuwa nchi mfano sio tu Afrika bali duniani kwa ujumla.

Mauritius ambayo ni nchi ya kisiwa iko nafasi ya nne kwa usafi Afrika na pia ni nchi yenye kuvutia watu wengi kwa vigezo kadhaa zikiwa fukwe nzuri na za kuvutia ambapi pia ni nchi nzuri kwa shughuli za kibiashara.

Kwa sasa Mauritius inashika nafasi ya nne Afrika kwa usafi kulingana na utafiti ikishika nafasi ya 81 duniani.

Changamoto nyingine ni taka kutoondoshwa kwa wakati katika mitaa kutokana na ukosefu wa wazabuni au vikundi vyenye nyezo za uhakika na uhaba wa vyombo vya usafiri kwa ajili ya uondoshaji wa taka.

Bado kuna changamoto kwa taka zinazozalishwa kutokana na huduma za afya katika baadhi ya maeneo vikiwemo vituo vya kutolea huduma ya afya  ambapo udhibiti taka hatarishi unahitajika kwa kujenga vichomea taka katika hospitali na vituo vya afya jambo ambalo hata zile hospitali na vituo vya afya binafsi vinatakiwa kulifanyia kazi.

Kuna haja ya kuwekwa utaratibu wa kudhibiti utupaji taka ovyo barabarani baada ya watu kula vyakula au vinywaji wawapo safarini na kurembea barabara tabia ambayo imezoeleka kwa baadhi ya wananchi.

Mipango ya jamii kudhibiti taka katika maeneo yao inaunga mkono uundaji wa mzunguko wa uchumi anasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake mahususi kwa ajili ya Siku ya Kimataifa ya Makazi anasema kuwa “juhudi za umma za kupanua maeneo safi ya kijani yanasaidia kupoza maeneo ya mijini nyakati za mawimbi ya joto.”

Usafi  iwe kwa watu wote au kwa mtu mmoja mmoja, unahitajika kisheria na mwanadamu anapaswa kuufanyia kazi kwa kila kitu kwani  ni katika mambo ambayo hulinda afya ambayo ni katika neema ya Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu.

Wanachuoni wameeleza umuhimu wa usafi wa majumbani pamoja na maeneo ya umma, ambapo usafi wake unahitajika zaidi kuliko kuupuuza kwani kuupuuza usafi kunapelekea madhara ya kiafaya kwa umma.