MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema nchi haiendeshwi kwa majaribio ya viongozi.
Kauli hiyo ameitoa jana wilayani Bunda mkoa wa Mara, alipozungumza kwenye mkutano wa kampeni za kuwania uras katika uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka huu.
Aliwaeleza wanaCCM na wananchi kwa ujumla kwamba katika uendeshaji wa nchi hakuna majaribio, bali viongozi wenye uzoefu ndio wanaopaswa kuwa na nafasi kuendelea na majukumu ya kuongoza nchi.
Dk. Samia alisema chama pekee chenye uwezo wa kiuongozi ni CCM na kwamba wasijejaribu kuwapa kura viongozi kutoka vyama vyengine.
Alieleza kuwa Chama cha Mapinduzi ndicho chenye viongozi waliopikwa kwa kufunzwa na kwamba wanauwezo wa kusimamia maslahi ya nchi, hivyo wahakikishe wanawapigia kura wagombea wote wa CCM.
Alisema wakiwapa kura wapinzani watakwenda kuzungumza na nani? Watakwenda kuomba barabara, maji na huduma nyengine kwa nani?
Alitoa wito kwa watanzania na wanaCCM wajitokeze kwa wingi Oktoba 29 mwaka huu, kwenda kupiga kura, kwa sababu CCM inategemea ushindi kutokana na mtaji wa wanachama, mashabiki na wapenzi wa chama hicho.
Akigusia maendeleo ya wilaya ya Bunda alisema kuna maendeleo makubwa yaliyopatikan katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Alisema kwenye sekta ya afya, serikali imejenga zahati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri, hospital ya wilaya na kwamba mpango uliopo ni kujenga hospitali za rufaa.
Alieleza akipata ridhaa serikali itashughulikia changamoto ya upatikanaji wa maji katika mji wa Bunda na kwenye vitongoji vyote vya mji huo.
Kwenye sekta ya kilimo alisema serikali itaongeza ujenzi wa skimu za umwagiliqji maji, sambamba na kuendelea kutoa ruzuku za mbolea na pembejeo za kilimo ili wakulima wazalishe kwa tija.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Steven Wasira, wakati akimkaribisha Dk. Samia, alisema Bunda ndio nyumbani kwao na kituo chake cha kupiga kura kipo hapo.
Aliwaambia wananchi wa Bunda kuwa amewapelekea mgombea urais mwenye uzoefu na sio mgombea uraisi wa majaribio kwani tangu awe madarakani ametekeleza mambo makubwa ya kimaendeleo.
Nae mgombea ubunge wa jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya, alisema wana kila sababu ya kwenda kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu ili wakampatie ushindi wa kishindo Dk. Samia Suluhu Hassan.
