Skip to content

Tutaleta madiliko ya maendeleo Rufiji – Dk. Samia

  • Bara

NA MWANAJUMA ABDI, RUFIJI

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema akichaguliwa kuwa rais, serikali itajenga mabwawa yatakayozuia mafuriko katika wilaya ya Rufiji.

Dk. Samia ameyaeleza hayo Ikwiriri wilaya ya Rufiji, mkoa wa Pwani katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Alisema serikali inakusudia kujenga mabwawa mawili makubwa na ujenzi wa zuio maji katika bonde la mto Rufiji, hatua ambazo zitaondosha kabisa mafuriko wakati wa mvua.

Alisema ujenzi wa mabwawa hayo utakwenda sambamba na utengenezaji wa skimu za kilimo cha umwagiliaji maji ambapo hekta 60, 000 imepangwa kuingizwa kwenye mpango huo.

Aliongeza kuwa serikali itajenga zuio la mafuriko litakalogharimu shilingi bilioni 245, barabara ya kilomita 90 na makalvati ambapo mkandarasi wa ujenzi huo ameshapatikana.

Dk. Samia alisema miradi ya kilimo imeongeza uzalishaji wa mazao ya chakula katika wilaya hiyo umeongezeka katika msimu huu kutoka tani 87,829 hadi tani 112,118 na mazao ya biashara la korosho uzalishaji umeongezeka kutoka kilo milioni 2.5 hadi kilo milioni 4.2.

Akizungumzia sekta ya uvuvi, alisema serikali imepeleka boti mbili za doria ambazo zimesaidia kupunguza uvuvi haramu kutoka asilimia 70 hadi asilimia 30 na kwamba hivi kumeshuhudiwa ongezeko la samaki waliovuliwa kutoka tani 600,000 hadi tani 900,000.

Kuhusu nishati ya umeme, Dk. Samia alisema wilaya ya Rufiji na Chalinze Mkoa wa Pwani ambapo kuna mradi mkubwa wa bwawa la Julius Nyerere watanufaika na mradi huo, hivyo wahakikishe wanalinda vyanzo vinavyotiririsha maji katika bwawa hilo.

Alisema katika sekta ya kuwezesha wananchi kiuchumi takwinu zinaonesha serikali imetoa shilingi bilioni 3.4 kwa vikundi 502, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa vikundi hivyo.

Dk. Samia aliwaomba wananchi wa Ikwiriri, wilaya ya Rufini na mkoa wa Pwani kuhakikisha wanawapigia kura wagombea waliosimamishwa na Chama cha Mapinduzi ili wakasimamie maendeleo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha- Rose Migiro alisema wilaya hiyo inahitoria kubwa ya maendeleo katika sekta mbali mbali za huduma za kijamii na kiuchumi chini ya uongozi wa Dk. Samia.

Aliwataka wananchi wa Ikwiriri na maeneo mengine wahakikishe wanakwenda kuwachagua viongozi waliosimamishwa na Chama cha Mapinduzi, ambao ndio wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo.

Nae Mgombea Ubunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa alisema Tanzania inakwenda kuandika historia ya mpya ya mapinduzi wa kiuchumi na Rais wa kwanza mwanamke kupigiwa kura katika uchaguzi mkuu utaofanyika Oktoba 29.

Aliongeza kusema kuwa Rufiji wakati anaingia madarakani Dk.Samia kulikuwa na skuli nne na sekondari lakini sasa zimejengwa 22 na msingi zilikuwa 19 na sasa zipo 63.