Na Saida Issa, DODOMA
Tarehe 21 Machi ya kila mwaka huadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Down Syndrome, siku iliyoidhinishwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 2011 kwa lengo la kuongeza uelewa, kutambua mchango wa watu wenye hali hii duniani, na kutoa fursa kwa mataifa kutafakari nafasi yao katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Akizungumza jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Kizito Wambura, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye Down Syndrome, wanapata huduma bora na fursa sawa katika jamii.
Amebainisha kuwa Serikali imeweka mifumo madhubuti ya kisheria na kisera, ikiwemo Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sera ya Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo, ili kulinda haki na ustawi wa kundi hilo.
Aidha, Wambura amesema watu wenye Down Syndrome wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia sekta mbalimbali kama elimu, sanaa, michezo na shughuli za kijamii na kiuchumi. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa jamii kuwatambua, kuwaheshimu na kuwawezesha kikamilifu ili washiriki ipasavyo katika maendeleo ya nchi.
“Ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha tunajenga jamii yenye usawa, haki na mshikamano bila ubaguzi,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha elimu jumuishi, kutoa vifaa saidizi, kuwajengea uwezo walimu, kuboresha miundombinu ya shule, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu kupitia halmashauri mbalimbali nchini.
Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hii, ambapo maadhimisho hufanyika katika halmashauri zote nchini. Kwa mwaka huu, viongozi wa kitaifa wa chama cha watu wenye Down Syndrome wanatarajiwa kukutana Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Tuwe Pamoja Dhidi ya Upweke” inalenga kuhamasisha mshikamano na ushirikishwaji wa watu wenye Down Syndrome katika jamii.
Siku hii pia inatambua mchango wa Dkt. Langdon Down aliyegundua hali ya Down Syndrome, na inalenga kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu haki za watu hawa, ikiwemo haki ya elimu, ajira, huduma za afya na ushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa, watu wenye Down Syndrome wanastahili kuishi kwa kujitegemea ndani ya jamii, kupata elimu jumuishi, kushiriki katika ajira, pamoja na kushiriki kikamilifu katika utamaduni, michezo na burudani.
