NA HAFSA GOLO
AJIRA ni jambo muhimu katika mustakabali wa mfumo wa maisha na ndio msingi katika maendeleo ya taifa lolote.
Kupitia ajira,vijana hutumia elimu na ujuzi wao kuchangia kukuza uchumi na kuongeza uzalishaji.
Pia ajira mara nyingi huwajenga vijana kimaadili kwa kwafundisha uwajibikaji na kushirikiana na watu wengine hali hii husaidia kupunguza changamoto za kijamii kama uhalifu na utegemezi.
Waziri wa Vijana ,Ajira na Uwezeshaji Shaaban Ali Othman akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alieleza kuwa lengo la serikali kuunda wizara hiyo,ni kuwaimarishia vijana kiuchumi na kijamii,kwa kwapatia fursa za ajira, ujasiriamali na maendeleo kupitia vipaji vyao.
Alisema kuwa Wizara ya Vijana,Ajira na Uwezeshaji Zanzibar ilianzishwa Novemba 13 mwaka 2025 kutokana na takwa la kisheria kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya 1984 chini ya ibara 42(1)
Alifahamisha kuwa wizara hiyo, iliundwa kwa kujumuisha sekta ya vijana,ajira na uwezeshaji kufuatia umuhimu wake wa kuwaunganisha vijana ,kubuni na kusimamia mipango na taratibu za soko la ajira ili kuimarika kwa fursa za ajira nchini.
Vile vile,alieleza wizara hiyo ina jukumu la kuhakikisha kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 katika kufikia malengo ya kuzalisha ajira na kuwainua vijana kiuchumi.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ipo sambamba na kufikia malengo ya mpango mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kuweza kuajiriwa na kujiajiri.
MAJUKUMU YA WIZARA
Akizungumzia kuhusu majukumu ya wizara alisema kuwa serikali imeipangia kusimamia na kuratibu shughuli za uendeshaji na Utumishi,kuratibu mipango ,sera na utafiti katika masuala yanayowahusu vijana ,ajira na uwezeshaji.
“Muundo huu ni muhimu kwa Wizara na Taasisi zake katika kufanya kazi kwa dhamira iliyokusudiwa na kutoa matokeo chanya yanayoratibiwa kwa umma,”alisema.
Alitaja majukumu mengine ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera na mipango ya sekta,kufanya na kuhamsisha tafiti zinazohusiana na maendeleo sekta na kusimamia usimamizi wa rasilimali watu ,fedha na nyenginezo.
“Jukumu jengine tunalosimamia ni kuhakikisha kukuza na kuwezesha uwezeshaji wa kiuchumi kwa wananchi kupitia utoaji wa mikopo,ruzuku ,mafunzo na huduma na kukuza biashara ndogo na zakati”,alieleza.
Alibainisha juhudi hizo zipo sambamba na suala la kuanzisha na kukuza upatikanaji wa ajira kwa vijana,kubuni mikakati ya kuongeza fursa za ajira,kusimamia na kukuza vyama vya ushirika na kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana.
“Jukumu letu jengine ni kusimamia haki na stahiki za vijana,kuanzisha na kukuza program mbambali za maendeleo yao pamoja na kuzisimamia shughuli zote zinazofanywa na baraza la vijana”,alieleza.
MALENGO YA WIZARA
Alifahamisha lengo kuu la Wizara hiyo alisema ni pamoja na kuwawezesha vijana,kukuza ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi kwa kuzingatia sera,sheria mikakati ya kitaifa ikiwemo Ilani ya CCM na Dira ya Maendeleo ya Taifa na Kimataifa.
“Mapngo huo utasaidia kufikia malengo endelevu na Afrika tuitakayo ifikapo 2063,”alisema.
Aidha alisema kuwa kupitia Idara ya Ajira ,jumla ya ajira za ndani 2,553 zimeratibiwa kupatikana ambapo kati ya hizo wanaume ni 1,579 na wanawake 974.
Alifafanua kuwa ajira hizo zimetokana na sekta mbalimbali zikiwemo hospitali,hoteli,vituo vya mafuta pamoja na skuli.
Akizungumzia ajira za nje nchi alisema wananchi 735 walipata fursa hizo,wakiwemo wanaume 247na wanawake 488,aidha mahafali ya vijana 20 yaliratibiwa na wizara hiyo.
“Wananchi walipata ajira hizo kupitia Mawakala Binafsi wa Ajira katika nchi ya Oman,Kuweit,Qatar ,Saudia –Arabia na UAE kwa kazi za vibarua ,udereva hoteli na kazi za majumbani”,alisema.
Alibainisha kuwa kwa upande wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA)alisema jumla ya mikopo yenye thamani ya 4,161,157,560 ilitolewa kwa wananchi wapatao 1072 kati ya hao Unguja 831 na Pemba 241.
Aliongeza Waziri Shaban kwamba makusanyo ya marejesho ya mikopo alisema ni jumla ya shilingi 2,070,501,866.11zilikusanywa ikiwa Unguja 152,505,601 na Pemba 716,417,324.
Alifahamisha kuwa hatua hiyo ipo sambamba na uazishaji wa shamba darasa kwa wafugaji wa nyuki kisiwani Pemba,kutengeneza moduli mbili za kufundishia ujasiriamali kwa bidhaa za urembo na kilimo cha kisasa cha mboga mboga na kutoa mafunzo kwa wananchi 743.
“Katika mafunzo hayo Unguja wanchi 386 na Pemba 357 walipatiwa kupitia fani ya upambaji,usarifu wa viungo,ujasiriamali,ushonaji,usimamizi wa fedha na kilimo cha mboga mboga “,alieleza Waziri Shaban.
Pia alisema jumla ya wajasiriamali 31 walipata fursa ya kushiriki maonesho kwa ajili ya kutangaza bidhaa zao,kuuza na kuwajengea uwezo ambapo kati ya hao wanawake walikuwa 23 na wanaume wanane.
Akizungumzia kuhusu mafanikio yaliopatikana kupitia Baraza la Vijana alisema, kuwa vijana 82 walipatiwa mafunzo ya Komputa katika kituo cha TEHAMA cha Machomanne na kituo cha Ubunifu Pujini huku vijana 196 walipatiwa elimu ya mazingira kupitia mradi wa mabadiliko ya tabianchi.
Aidha Waziri huyo alisema kuwa pamoja na hatua hiyo iliyopatikana katika kipindi kifupi juhudi za kuimarisha maendeleo ya vijana kiuchumi zinaendelea kuchukuliwa kwa kuibua miradi mbalimbali.
KAZI ZA TAASISI NA VITENGO
Akizungumzia baadhi ya kazi zinazofanywa na taasisi na vitengo mbali mbali vilivyomo ndani ya wizara hiyo alisema kuwa Idara ya Uendeshaji na Utumishi imekuwa ikisimamia utoaji wa huduma za uendeshaji na utumishi kwa kusimamia maslahi ya rasilimali watu.
IDARA YA MIPANGO NA UTAFITI
Alisema miongoni mwa majukumu ya idara hiyo ni kutayarisha na kuzifanyia mapitio sera,kufanya tafiti sambamba na ufatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi huku kuwandaa program za miradi.
IDARA YA MAENDELEO YA VIJANA
Alisema kuwa Idara hiyo, imekuwa ikifanya kazi ya kuwahamasisha,kuwapa mafunzo na kuvisaidia vikundi vya ushirika kwa kuwawezesha kiuchumi kwa kujiajiri kupitia sekta mbalimbali
IDARA YA AJIRA
Alifahamisha kuwa kutokana na umuhimu wa eneo hilo kwa vijana idara hiyo, hufanyakazi za kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera ya ajira na mpango wa utekelezaji wa ajira kwa vijana.
Alisema lengo ni kuimarika kwa mazingira na fursa za ajira nchi.
WAKALA WA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI ZANZIBAR (ZEEA)
Alifahamisha kuwa eneo hilo linajukumu ya utoaji wa mikopo isiyo na riba ,mafunzo ,ukuzaji biashara na teknolojia.
“Hapo huandaliwa mazingira rafikia ya utoaji wa mafunzo na mambo mengine muhi ambayo yatachangia kupunguza vikwazo kwa wafanyabiashara”,alisema.
CHANGAMOTO
Licha ya mafanikio hayo bado alisema wizara hiyo inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti ya utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo linachelewesha kutimiza malengo kwa wakati.
“Tumekuwa tukichukuwa juhudi za kushirikiana na wadau wa mbali mbali katika kutekeleza majukumu kama vile UNICEF, UNDP, ILO, UNFPA, UN-WOMEN NA JICA”,alieleza.
Alifaja changamoto nyengine ni pamoja na uhaba wa vyombo vya usafiri jambo linalokwamisha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa.
Pamoja na hilo,alisema miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa ili kumaliza changamoto hiyo alisema ni kushirikiana na serikali kwa ajili ya kupatiwa magari huku akisema upo mpngo wa kufanya manunuzi ya gari sita na honda 10 Unguja na Pemba.
Hata hivyo,Waziri huyo alisema kuwa kutokana na kufanya kazi kwa mashirikiano kumechangia kupiga hatua ya mafanikio katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwa wizara hiyo.
Aliwaomba watendaji na viongozi kuendelea kushirikiana, kubadilishana uzoefu,kufuata sheria na kufanyakazi kwa bidi ili kuifikia kasi ya serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk.Mwinyi.
Alisema kuwa kusimamia na kufuata misingi ya utumishi wa umma pamoja na kuweka kipaumbele cha uzalendo itasaidia kutimiza ndoto za serikali katika kipindi kifupi kijacho hasa katika suala zima la uzalishaji wa ajira mpya nchini.
