Skip to content

Serikali yatoa bilioni 10.5 kuwawezesha wafanyabiashara

  • Bara

Na Saida Issa, Dodoma

NDANIya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, kiasi cha shilingi bilioni 10.5 kimetolewa kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo zaidi ya 100,000 waliokwisharasimishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kujenga uchumi jumuishi unaowashirikisha wananchi wengi zaidi katika shughuli za kiuchumi.

Alifafanua kuwa sekta isiyo rasmi ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kwa kutoa ajira kwa mamilioni ya Watanzania, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Pamoja na umuhimu wake, sekta hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa usajili wa kisheria, mitaji, masoko pamoja na huduma za ulinzi wa kijamii,

Kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua za kuimarisha urasimishaji wa wafanyabiashara ndogondogo ili kuwaingiza katika mfumo rasmi wa uchumi,

Hadi sasa, wafanyabiashara 119,595 wamesajiliwa kupitia Mfumo wa Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBN–MIS), huku zoezi la utambuzi, usajili na uwezeshaji likiendelea katika sekta mbalimbali nchini,”alisema.

Dkt. Gwajima alieleza kuwa kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1.35 zimetolewa kupitia Benki ya NMB kwa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 7 kwa wafanyabiashara mmoja mmoja, wanawake na wanaume, Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unaendelea kutoa mikopo kwa riba ya asilimia 4.

“Kupitia TAMISEMI, zaidi ya vikundi 6,000 vimenufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 33,

Vilevile, Serikali kupitia taasisi mbalimbali zikiwemo SIDO, PPRA na TAMISEMI imeendelea kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia mafunzo, leseni na fursa za masoko ikiwemo kushiriki katika zabuni za Serikali,”alisema.

Alieleza kuwa Kwa upande wa sekta ya fedha, benki mbalimbali ikiwemo NMB, TCB na DCB zimetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa wafanyabiashara waliorasimishwa.

Kwa ujumla, uwekezaji wa shilingi bilioni 10.5 umechochea maendeleo ya wafanyabiashara ndogondogo, kuimarisha sekta isiyo rasmi na kuweka msingi imara wa uchumi jumuishi na shindani,Serikali imeendelea kuwasisitiza wananchi kurasimisha biashara zao ili kufaidika na fursa mbalimbali zinazotolewa.