NA HAFSA GOLO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatarajia kutumia shilingi bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa skuli nne za kisasa za ghorofa mbili zitakazohudumia elimu ya msingi na sekondari katika wilaya za Mjini na Magharibi ‘A’.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdalla Said, alisema fedha hizo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, huku ujenzi wa skuli hizo ukitarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema lengo la ujenzi huo ni kutekeleza ahadi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, za kuimarisha miundombinu ya elimu na kuondoa msongamano wa wanafunzi katika madarasa.
Aidha, alisema serikali inaendelea kusimamia mikakati ya uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora katika mazingira rafiki na salama.
“Elimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, hivyo serikali itaendelea kuwekeza katika miradi itakayowanufaisha wananchi moja kwa moja”, alisema Katibu Mkuu huyo.
Sambamba na hilo, alisema wizara tayari imeshasaini mikataba ya ujenzi na kampuni mbili za Tanzania ambazo ni FASTER na TILL, ambapo Februari 6, mwaka huu, wakandarasi hao walikabidhiwa rasmi maeneo ya ujenzi ili kuanza utekelezaji wa mradi huo.
“Hivi karibuni (Februari 6) tumewakabidhi rasmi wakandarasi maeneo ya ujenzi kwa ajili ya kuanza kazi. Hii ni hatua muhimu ya utekelezaji wa mipango ya serikali na ahadi za Dk. Mwinyi za kuimarisha mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji”, alisema.
Alifahamisha kuwa Kampuni ya TILL kutoka Dar es Salaam itajenga skuli za msingi za Kianga na Mtoni zilizopo Wilaya ya Magharibi ‘A’, huku Kampuni ya FASTER ya Zanzibar ikijenga skuli ya sekondari ya Jang’ombe pamoja na Mikunguni katika wilaya ya Mjini.
Vilevile alisema Mshauri elekezi wa mradi huo ni kampuni ya wahandisi waliobobea katika usimamizi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo aliwasisitiza wakandarasi hao kuwa na mpango kazi mzuri utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kukamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa.
“Nawaomba mtambue kuwa mradi huu unalenga kuimarisha miundombinu ya elimu na kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa unaotokana na ongezeko la wanafunzi katika maeneo haya”, alieleza na kuongeza kuwa ni muhimu utekelezaji wa majukumu yao uzingatie weledi na viwango vya ubora.
Pamoja na hayo, aliwaomba wananchi kuupokea mradi huo kwa matumaini makubwa, akieleza kuwa utasaidia kuondoa mfumo wa mikondo miwili, kuongeza ubora wa elimu kwa watoto wao na kutoa suluhisho la kudumu la kupunguza msongamano katika madarasa.
