Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeishauri Menejimenti na Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kuangalia uwezekano wa kuwekeza miradi ya maendeleo Zanzibar ili kuongeza kasi ya maendeleo ya mfuko na nchi kwa ujumla.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Saada Mkuya Salum, alitoa ushauri huo juzi alipomuwalkilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika futari iliyoandaliwa na mfuko huo kwa wanachama, wadau na wananchi katika hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege, iliyohudhuriwa pia na Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi na Mahusiano), Deus Sanga.
Dk. Mkuya alisema serikali ya awamu ya nane inahimiza uwekezaji kutoka sekta za umma na binafsi hivyo mfuko huo inaweza kutumia uzoefu ilionao kuwekeza Zanzibar hasa katika sekta za uchumi wa buluu na nishati.
Aliongeza kuwa hatua hiyo sio tu itaongeza ukwasi wa mfuko huo bali utaimarisha uwezo wake wa kuwahudumia wanachama wake na kurejesha kwa jamii kama ilivyofanya kwa taasisi mbalimbali za watu wa makundi maalu.
Aidha aliipongeza taasisi hiyo kwa kuamua kuwakutanisha wadau wake na makundi mbalimbali ya jamii hatua aliyosema inaongeza imani ya wadau hao kwa mfuko na kuimarisha ufanisi.
Vilevile aliipongeza kwa kuamua kutoa msaada wa fedha kwa jumuiya za watu wenye ulemavu na inayoihusika na watu wenye mazingira magumu hatua itakayoongeza ufanisi wa taasisi hizo.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, mkurugenzi mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, alieleza kuwa katika kutekeleza mpango wake wa kurejesha kwa jamii, mfuko huo umetoa shilingi milioni 30 kwa Chama cha Watu wenye Ualbino Zanzibar (ZAAO), Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB) na Life Lift Organization kama njia ya kuonesha shukrani.
Aidha alisema mfuko huo unaendelea kushiriki kwa vitendo katika uchumi wa Zanzibar kupitia michango yake katika miradi mikubwa, ya kati na mengine ya kijamii sanjari na kutoa huduma kwa wanachama wake ambao ni wastaafu na waajiri waliopo Zanzibar.
“Tunapongeza ushirikiano tunaoupata kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hatua inayotupa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika uchumi na maendeleo ya Zanzibar lakini pia kutoa huduma bora kwa wanachama wetu”, alieleza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Waziri Sangu, alimshukuru Dk. Mwinyi, wadau na wanachama wa mfuko huo kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tukio hilo jambo linaonesha mshikamano na ukaribu baina ya taasisi hiyo na wadau wake.
Aidha Sangu alimuomba Dk. Mkuya kufikisha salamu za shukrani na zawadi maalum kutoka kwa Menejimenti na Bodi ya PSSSF kwa Dk. Mwinyi huku akiahidi kuwa wizara yake itaendeleza ushirikiano uliopo kama njia ya kuimarisha muungano wa Tanzania.
Wakizungumzia msaada waliopatiwa, Katibu wa ZAAO Mohammed Abdallah na Mkurugenzi wa Life Lift, Mtumwa Mohammed, waliipongeza PSSF kwa kuwapatia fedha hizo walizosema zitasaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Aidha walitoa wito kwa taasisi myengine za umma na binafsi kuweka mpango mahsusi wa kuziwezesha taasisi zinazoshughulika na watu wenye mahitaji maalum hasa wenye ulemavu kwani wana changamoto nyingi zinazokwanza kufikiwa kwa malengo ya taasisi hizo.
